NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imeitaka sekta Binafsi Tanzania kutumia fursa ya maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kufanya biashara na kuongeza mapato ya taifa kuinua uchumi wa nchi.
Aidha, mamlaka hiyo imesema uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya DP World na Adan umewezesha muda wa kupakua shehena bandarini hapo kupungua, hivyo kupunguza gharama za meli kusubiri na wafanyabiashara kunufaika zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus amesema maboresho yaliyofanywa yamekidhi vigezo, mahitaji na matarajio ya wafanyabishara na kuiweka bandari kwenye ushindaji wa kimataifa.
Gallus ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa amesema uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye miundombinu kama eneo la upakuaji na upakiaji mizigo kwa kutumia vifaa vya kisasa, ambapo kazi hiyo kwa sasa inafanyika ndani ya muda mfupi tofauti na hapo awali.
“Mashine za kupakia na kushusha mizigo yaani ‘Cranes’ zimerahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi mkubwa bandarini hapa. Ni nafasi ya pekee kwa sekta binafsi kuchangamkia,” amesema Gallus.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema TPA ina mpango wa kujenga bandari kavu (ICDs) katika eneo la Shimo la Udongo Kurasini jijini hapa kwa ajili ya kuhifadhia mizigo inayoharibika kwa haraka (perishable goods) kama vile matunda katika vyumba maalum vyenye ubaridi.
“Huko nyuma, mizigo ya bidhaa zinazowahi kuharibika ilikuwa inapitia katika bandari ya nchi jirani, lakini hivi sasa mizigo hiyo itakuwa inahifadhiwa katika bandari kavu ikisubiri kusafirishwa kwenda nje ya nchi,” amesema.
“Kufuatia maboresho tuliyoyafanya, hivi sasa hakuna tena malalamiko ya kuchelewa kutolewa kwa mizigo inayowasili bandarini na badala yake, kutokana na kasi ya utendaji iliyopo, wateja ndio wanaochelewa kuja kuchukua mizigo yao,”
Amesema TPA ina maeneo makubwa ya kuhifadhi mizigo na kutoawito kwa wafanyabishara kuchukua mizigo yao kwa wakati bandarini kwani bandari siyo sehemu ya kuhifadhi mizigo kwani mizigo yote ya wateja inatakiwa itoke ili kutoa nafasi kwa mizigo mingine.
“Kasi ya ushushaji wa shehena itaboreka zaidi wateja watakapochukua mizigo yao kwa wakati," amesema Gallus na kuongeza kuwa TPA imejipanga na itaendelea kuwa lango imara la uchumi.
Gallus amesema kwa sasa bandari ina uwezo wa kushusha makasha 1000 kwa siku moja na kwamba DP World wanatarajia kufunga mtambo mpya ambao utawesesha kushusha makasha 1,500 kwa siku.
Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, Elitunu Mallamia amesema kinachotokea sasa hivi katika bandari ya Dar es Salaam ni mizigo kusubiri wateja kuondolewa na siyo uchelewashaji tena kutokana na kasi ya utendaji iliyopo .
"Tumeweza kuhudumia shehena zaidi ya asilimia 25 kwenye miezi hii ambayo tumefanya kazi kuanzia mwezi Mei 2024 mpaka sasa Januari 2025)," amesema Mellamia.
Amesema kwa mwezi Desemba pekee magari 25,251 yalishushwa kwenye meli 16 na kuvunja rekodi, huku akiweka bayana mipango yao ni kuhakikisha wanatoa huduma ambayo itapita lengo la serikali la kuhudumia mzigo wa tani milioni 30.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Tanzania, Hamis Livembe aliipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuleta mageuzi makubwa kwenye bandari zote hapa nchini.
“Miaka miwili iliyopita, tulikuwa na kilio cha ucheleweshwaji wa mizigo kutoka bandarini na wakati mwingine biashara zilichelewa kuwafikia wateja kwa wakati ila kwa sasa sisi ndio tunachelewa kuchukia mizigo," amsema.
Mwenyekiti huyo amesema maboresho yaliyofanyika na uwekezaji wa DP World na wengine umeweza kupunguza gharama za kutoa mzigo bandari kutoka dola za Marekani 8,000 hadi 3,000 hivyo kuitaka serikali iendelee kufanya maboresho.
"Kuna kipindi tulikuwa kutoa mzigo hapa ilifikia milioni 20 kwa kontena moja ila kwa sasa haizidi milioni 7 haya ni mafanikio makubwa sana, tunampongeza Rais Samia kwa kuwaleta wawekezaji hawa wawili kwani sisi tunafaidika, " amesema.
Akizungumzia changamoto ya bei za bidhaa zinazopitia bandari ya Dar es Salaam Livembe alisema kwa sasa sababu ni gharama za usafiri, kodi mbalimbali na kupanda na kushuka kwa dola ya Marekani, huku akisisitiza kuwa wanaendelea kujadiliana na serikali ili kupungua kodi zisizo na sababu.
No comments:
Post a Comment