NA MWANDISHI WETU
BARAZA Kuu la Uongozi la Taifa
(BKUT) la CUF- Chama Cha Wananchi, limetoa maagizo kwa Katibu Mkuu na Manaibu
wake kuendeleza kazi ya kukamilisha Ilani ya Uchaguzi wa Tanzania Bara na
Zanzibar itakayozingatia maoni ya Haki Sawa na Furaha kwa Wote ambayo
yameingizwa katika Dira ya Taifa 2050.
Maoni pia yanajikita Kuunda
Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayokamilisha upatikanaji wa Katiba Mpya yenye
misingi imara ya demokrasia inayotokana na maoni ya wananchi.
Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti
wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akitoa taarifa ya Baraza
Kuu la Uongozi, kilichofanyika jijini Dar es Salaam Jan 8 hadi 9, 2025 ambapo pia
amewataka wajumbe wa baraza hilo kwenda kusimamia rasilimali za nchi ili ziweze
kuwa na manufaa na wananchi wote.
"Wajumbe wa Baraza Kuu ndio
viongozi wa kusimamia sera ya CUF ya haki sawa na furaha kwa wote, hivyo
nawaomba wakati tukiunda kamati ya kuandaa Ilani muipe ushirikiano wa hali na
mali ikiwa kuhakikisha ilani yetu inakuwa bora," amesema.
Lipumba amesema CUF ndio chama
kinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa nchi na jamii, hivyo ni vema ilani yao
ikidhi vigezo muhimu katika kuleta mabadiliko.
Amesema katika uandaaji wa
ilani hiyo watatumia ilani iliyopita kuangalia yale ambayo yanapaswa kuingizwa
nkwa kuongoza nguvu kazi ya kusimamia rasilimali .
Aidha aliwataka wajumbe hao wa
Baraza Kuu kuhakikisha wanatoa elimu na kuhamasisha wananchi umuhimu wa kupata
Katiba Mpya ambayo itagusa mahitaji ya wananchi.
"Napenda kutumia nafasi
hii ya kikao cha Baraza Kuu la chama kuomba kila mmoja ashiriki kikamilifu
katika kuhakikisha Ilani ya CUF 2025 inakuwa yenye ubora, lakini kubwa zaidi
nawaomba tupiganie Katiba mpya kwani ndio inaweza kuondoa changamoto zote
ambazo zipo nchjni ikiwemo uchaguzi," amesema.
Mwenyekiti huyo amesema chama
chao kinatarajia kuja na ilani ambayo itaunganisha wananchi na viongozi wake
ili kuchochea maendeleo.
Lipumba amesema Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa umeonesha namna ambavyo Katiba ya sasa inavyochangia kuzuia
haki za wananchi kuchagua, hivyo ni wakati muafaka kwa kila mpenda haki sawa na
furaha kwa wote kushiriki kudai Katiba Mpya.
Mwenyekiti huyo ameweka wazi
iwapo wananchi watawapa ridhaa ya kuingoza Tanzania 2025 watahakikisha kunakuwa
na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vyama vyote kushiriki kuunda Serikali.
Amesema hali ya maisha kwa sasa
ni ngumu jambo ambalo linapelekea vijana wengi kuonekana wazee, hivyo kuishauri
serikali kuwekeza kwa vijana.
Lipumba amesema sekta ya elimu
nayo imekuwa haina faida kwa vijana kwani bado ipo katika misingi ya kizamani
jambo ambalo linatakiwa kuangaliwa upya.
Kwa upande mwingine Lipumba
ameitaka serikali iboreshe sekta afya hasa katika eneo la mama wajawazito na
watoto kwani takwimu zinaonesha bado vifo ni vingi.
Amesema iwapo Serikali itatumia
rasilimali misitu, wanyama, ardhi, madini na nyingine Tanzania itapata
maendeleo ya haraka.
Aidha ameitaka Serikali
kuwekeza kwenye viwanda ili kuweza kulisha nchi jirani na kuongeza ajira.
Katika kikao hicho Husna
Mohamed Abdallah, amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya akichukua nafasi iliyoachwa
na Hamad Masoud Hamad ambaye hakugombea kutokana na kukosa sifa.
Pia kikao kimemchagua Magdalena
Sakaya kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Barana Alli Khamis akichaguliwa kuwa
Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar.
No comments:
Post a Comment