JAMII YATAKIWA KULINDA MRADI WA EACOP - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, January 12, 2025

JAMII YATAKIWA KULINDA MRADI WA EACOP


Mshauri wa Makabila ya watu wa pembezoni kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta la Africa Mashariki (EACOP) Dkt. Elifuraha (katikati aliyevaa suti) akiteta jambo na viongozi wa Kitaifa wa makabila ya watu wa pembezoni wakati wa mkutano wa nne wa robo mwaka uliofanyika jijini Arusha uliolenga kutoa elimu kwa viongozi hao juu ya maendeleo ya mradi.

NA MWANDISHI WETU, ARUSHA

VIONGOZI wa jamii ya watu wanaoishi pembezoni mwa miji, maarufu kama watu wa asili wamezitaka jamii zinazoishi maeneo ambayo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika mashariki (EACOP) unapita kuwa sehemu ya ulinzi wa rasilimali zinazotumika katika ujenzi huo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla


Wakizungumza wakati wa kikao cha nne cha robo mwaka kilichofanyika jijini Arusha na kulichowakutanisha viongozi wote wa mkabila ya jamii za Masai, Wa-akie, Wa-Bargaig pamoja na Wataturu, viongozi hao pia wamezitaka jamii zao na watu wengine wanaoishi maeneo ya karibu na mkuza kutochukua mabaki ya vifaa vya ujenzi huo kwa sababu sio salama kwa matumizi ya binadamu.


Mmoja wa viongozi hao, Petro Mayomba kiongozi wa kabila la Barbaing kutoka wilaya ya Hanang mkoani Manyara  amesema kuwa licha ya mradi kutoa elimu kila wakati katika maeneo yao kuhusu kuchukua tahadhari za usalama wakati wa ujenzi, jamii zao pia zinapaswa kuwa mamna moja katika ulinzi wa rasilimali za mradi huo.


“Sisi kama watu wa asili ni moja wa wanufaika wa mradi na ndio maana tunakaa na viongozi wa mradi mara moja kila baada ya miezi mitatu kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wake,”


“Tunajua sasa hivi mabomba yanasambazwa katika maeneo mbalimbali unakopita mkuza kwa ajili ya kuyafukia kwa kazi ya usafirishaji wa mafuta ghafi , hivyo tunaziomba jamii zetu kushirikiana na mradi kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa rasilimali hizi utakaotokea,”


“Lakini pia tunapaswa kuwa walinzi namba moja wa miundombinu hii ili mradi huu ukamilike na kuleta manufaa kwa taifa”, amesema mzee Mayomba.


Naye Kalolo Bato kiongozi wa kabila la Watatoga kutoka wilaya ya Igunga amesema kuwa wamekuwa wakielimishwa kuhusu kutotumia kitu chochote kinachopatikana kwenye maeneo yao kwa sababu sio salama kwa viumbe hai.


“Tunaziomba jamii zetu kutotumia kitu chochote kilichopo katika maeneo yao kwa ajili ya mradi kwa sababu vitu hivyo sio kwa matumizi ya binadamu au mifugo,”

 


“Licha ya uwepo wa ulinzi katika maeneo ya mradi, lakini sisi wenyewe pia tunapaswa kuchukua tahadhari ya kutotumia mabaki ya vifaa kwa sababu sio salama kwa matumizi,” amesema.


Elizabeth Masakoi wa kabila la Wamasai kutoka Handeni mkoani Tanga amesema mradi huu umekuwa ukiwapa fursa mbalimbali akina mama ikiwemo elimu ya ujasiriamali, hivyo ni muhimu jamii zinazozunguka maeneo ya mradi zikashirki kikamilifu katika ulinzi wa miundomninu yake.


“Tunaona watoto wetu wanapata ajira na sisi kama waguswa tunapewa elimu ya kilimo na ufugaji,”


“Hivyo, mradi huu umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii zetu za pembezoni na tuna amini utakuwa na faida nyingi pindi utakapokamilka kwa ajili yetu an taifa kwa ujumla,”


“Hivyo, kama sehemu ya waguswa, tunauthamini na kuzitaka jamii zetu kuwa walinzi wa miundombinu inayopita katika maeneo yao,”, amesema.


Mshauri wa makabila ya watu wa pembezoni kutoka EACOP Dkt. Elifuraha amesema kuwa mradi huo umekuwa ukiwashirisha watu wa jamii  hizo kama sehemu ya mafanikio ya mradi huu kupitia vikao vya mara kwa mara.


“Ili mradi ufanikiwe, unahitaji ushirikiano na jamii za pembezoni na ndio maana mradi kwa kiasi kikubwa umekuwa ukitoa kipaumbele cha fursa mbalimbali kwa jamii hizi ikiwemo ajira, elimu ya ufugaji na kilimo ili kuboresha maisha yao,” amesema.


Huu ni mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga huu una urefu wa jumla ya kilomita 1443, ambapo kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania.


Kwa upande wa Tanzania, bomba hilo linapita katika mikoa nane nane na wilaya ya 24.


Mikoa hiyo na wilaya zake katika mabano ni  Kagera (Bukoba Vijijini, Muleba na Biharamulo), Geita (Chato, Geita, Bukombe na Mbogwe),


Shinyanga (Kahama Mjini), Tabora (Nzega Vijijini, Nzega Mjini na Igunga), Singida (Iramba, Mkalama na Singida Mjini), Dodoma (Kondoa na Chemba),Manyara (Hanang na Kiteto) na Tanga (Kilindi, Handeni Mji, Handeni Vijijini, Korogwe, Muheza na Tanga Mji).


Wanahisa ni TotalEnergies yenye asilimia 62, wakati Mashirika ya Maendeleo ya mafuta (TPDC- Tanzania na (UPDC kwa upande wa Uganda ) yana miliki asilimia 15 kila moja na shirika la mafuta la  China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu katika mradi huu

 



No comments:

Post a Comment