BARRICK NI KIELELEZO BORA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI NCHINI- DKT. KIRUSWA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, February 15, 2025

BARRICK NI KIELELEZO BORA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI NCHINI- DKT. KIRUSWA


NA MWANDISHI WETU, KAHAMA

NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema kuwa Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu ya Barrick ni mfano bora wa uwekezaji nchini Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi wa nchi pamoja na namna inavyoendesha shughuli zake kwa uwazi na ufanisi.


Dkt. Kiruswa aliyasema hayo, Februari 15, 2025, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, uliopo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga. Ziara hiyo ililenga kujionea shughuli za uchimbaji madini na athari chanya zinazotokana na uwekezaji wa Barrick nchini.


Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa alibainisha kuwa Barrick si tu moja wa vinara katika sekta ya uchimbaji wa madini, bali pia inatekeleza kwa vitendo dhana ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), jambo ambalo limeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wanaoishi karibu na mgodi huo.


Dkt. Kiruswa, alieleza kuwa, mchango wa Barrick nchini Tanzania unaonekana kwani mchango wa Mapato kwa Serikali tangu kuanzishwa kwa ubia wa Twiga kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania mwaka 2019, kampuni hiyo imeingiza zaidi ya shilingi trilioni 11 katika uchumi wa nchi, ikiwa ni kipindi cha miaka 4 pekee kuanzia mwaka 2020 hadi 2024. 


Naibu Waziri Dkt. Kiruswa aliongeza kuwa, suala la ajira kwa Wananchi wa Tanzania Barrick imeajiri wafanyakazi 6,185 nchini Tanzania, ambapo asilimia 96 ni Watanzania. Kati ya hao, asilimia 53 wanatoka katika jamii zinazozunguka migodi ya kampuni hiyo, ikionyesha dhamira ya Barrick katika kuendeleza ajira za ndani na kuinua maisha ya wananchi wa maeneo husika. 


Dkt. Kiruswa alisisitiza kuwa, Kampuni ya Barrick inatekeleza miradi ya Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kwa ufanisi katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara, pamoja na ufundi stadi.


Kwa upande wake, Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda, alipongeza juhudi za Barrick kupitia mgodi wa Bulyanhulu kwa kushirikiana vyema na wananchi wa eneo hilo na kuihimiza kampuni hiyo kuendelea kuwekeza katika miradi endelevu itakayobaki kama alama ya maendeleo kwa jamii, hata baada ya shughuli za uchimbaji wa madini kukoma.


Mhe. Ng’enda alisisitiza kuwa utaratibu wa Barrick kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari na kuruhusu wananchi kuhoji na kutoa maoni yao ni kitendo cha kuigwa na Kampuni zingine ili kujenga mahusiano mema na jamii inayozunguka miradi yao.


Alisema kuwa, Kampuni zinazowekeza katika sekta ya madini zinapaswa kuiga mfano wa Barrick kwa kuhakikisha kuwa uwekezaji wao unaleta tija kwa jamii inayowazunguka kwa muda mrefu.


Naye, Meneja wa Mgodi wa Bulyanhulu, Victor Lule, alieleza kuwa mgodi huo umewekeza katika miradi mbalimbali ya kijamii inayolenga kuboresha maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa shule za msingi na sekondari zikiwemo tatu za vidato vya tano na sita pamoja na Chuo cha Uuguzi na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), ili kuwawezesha vijana kupata elimu bora na stadi za kazi, ambavyo vitawasaidia vijana kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.


Alisema kuwa Barrick kupitia Mgodi wa Bulyanhulu inatekeleza miradi ya usambazaji wa maji safi kwa jamii, Ujenzi wa barabara ya Kahama - Bulyanhulu - Kakola hadi yenye urefu wa kilomita 73 kwa kiwango cha lami, unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 101.2, ni hatua muhimu katika kuboresha usafiri na uchumi wa eneo hilo. Barabara hiyo itaongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa na huduma, na kuchochea maendeleo ya biashara na uwekezaji katika mikoa ya Shinyanga na Geita.





No comments:

Post a Comment