"HARAKISHENI MCHAKATO WA KUHAMISHA TUME YA TAIFA YA UNESCO" - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, February 12, 2025

"HARAKISHENI MCHAKATO WA KUHAMISHA TUME YA TAIFA YA UNESCO"

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Elimu, utamaduni na Michezo Mhe Husna Sekiboko (MB),  akiongoza semina ya juu chimbiko na majukumu ya Tume ya taifa ya UNESCO  iliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni naibu waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Omary Kipanga na  kushoto ni  katibu wa kamati na Mwenyekiti wa bodi ya Tume ya taifa ya UNESCO  Prof Elifas Bisanda.

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Elimu, utamaduni na Michezo, Mhe Husna  sekiboko  ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuharakisha mchakato wa kuihamisha Tume ya Taifa ya UNESCO  kutoka katika wizara hiyo kwenda ofisi ya Makamu wa Rais ili kuongeza ufanisi wa Tume hiyo. 


Akizungumza katika ufunguzi wa semina kwa Kamati ya Bunge juu ya chimbuko na majukumu ya Tume ya Taifa ya UNESCO iliyofanyika jijini Dodoma, Mhe. Sekiboko amesema kucheleweshwa kwa mchakato huo kunaleta changamoto za kiutendaji kwani Tume inashughulika na masuala mtambuka ya muungano yanayohusisha wizara tofauti tofauti huku ikiwa chini ya wizara isiyo ya muungano.


Awali wakichangia mada katika semina hiyo wajumbe wa kamati walitaka kujua kwanini wizara haijatekeleza maelekezo ya kamati ya kuhamisha Tume hiyo  kama kamati ilivyoagiza.


Akijibu maelekezo hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof. Carolyne Nombo amesema Wizara ilishaanza mchakato na kuahidi kuuongezea kasi ukamilike mapema.


 Akiwasilisha mada juu ya chimbuko na majukumu ya Tume ya Taifa ya UNESCO nchini, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Erick Kajiru amesema Tume hiyo ilianza kufanya kazi nchini mwaka 1962 ikiwa ni utekelezaji wa ibara ya saba ya katiba ya UNESCO na kupewa nguvu za kisheria mwaka 2008.



Ameeleza majukumu ya Tume kuwa ni pamoja na kuratibu, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa masuala ya UNESCO nchini,  kuwa kiungo cha mawasiliano na utekelezaji wa majukumu kati ya serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuhakikisha kuwa nchi yetu  inatekeleza majukumu yake yote ya uanachama wa  UNESCO. 


Ameyataja maeneo ambayo yanafanyiwa kazi na Tume kuwa ni pamoja na elimu, sayansi asili, sayansi jamii, utamaduni pamoja na habari na mawasiliano.


 Kajiru ametoa mifano ya masuala ambayo tayari Tume imeyafanyia kazi kuwa ni pamoja na kuratibu kutetea Pori la Akiba la Selous lisifutwe katika orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia. Aidha Tume iliratibu utetezi wa nchi na kufanikiwa kuondoa azimio la UNESCO la kuitaka Tanzania kusitisha ujenzi wa Mradi wa kufuata umeme wa Julius Nyerere katika Pori la Akiba la Selous. 


Hivi sasa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyo chini ya Katibu Mtendaji   Prof. Hamisi Malebo imejipambanua katika   kutetea maslahi ya nchi na kuchochea maendeleo katika masuala ya UNESCO kimataifa.


 Prof. Malebo wakati akifafanua kuhusu utendaji na majukumu yaliyotekelezwa na Tume, aliieleza Kamati kuwa masuala ya UNESCO ni ya Muungano na yanatekelezwa na Wizara ambazo siyo za Muungano kwa Tanzania Bara na Zanzibar.


 Pamoja na maelekezo hayo, Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuisimamia vizuri Tume ambayo imekuwa na ufanisi kiutendaji na imewezesha  sauti na msimamo wa Serikali katika masuala mbali mbali kusikika ndani ya nchi na katika duru za kimataifa.

No comments:

Post a Comment