CUF YASHTUKIA JANJAJANJA MUUNGANO VYAMA VYA SIASA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, March 2, 2025

CUF YASHTUKIA JANJAJANJA MUUNGANO VYAMA VYA SIASA


NA MWANDISHI WETU
               

CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa tayari ‘kimeshang’atwa na nyoka’ katika masuala ya kuunganisha vyama vya siasa ili kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu, hivyo hawataweza kuingia katika mtegoni huo.


Akizungumza na Waandishi jijini Dar es Salaam leo Machi 2, 2025 wakati akitoa msimamo wao kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amesema uchaguzi wa mwaka 2015 waliamini kuwa wanaunganisha vyama kwa dhati, kumbe chama kingine kipo kimkakati kudhoofisha vingine kutokana na uchu wa madaraka.


“Wakati ule tulipokuwa UKAWA, nikiamini tuko pamoja wakati na narudisha fomu ya kugombea kiongozi mmoja wa chama (jina kapuni) ambaye tulikuwa naye katika muungano huo alikuja kuniwekea pingamizi dakika za mwisho jambo ambalo liliniumiza sana,” alisema.


Pia aliongeza kuwa wakati wa ujazaji wa fomu kwa wagombea wa CUF, viongozi wa chama kingine (jina kapuni) waliwashawishi wajaze kama wanatoka kwenye vyama vyao na hiyo inadhihirisha walijipanga kudhoofisha vyama vingine.


Kulingana na changamoto hizo zilizojitokeza wakati huo wa kuunganisha vyama kwa lengo la kuwa na nguvu ya pamoja ili kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM), Prof Lipumba amesema kwa sasa wako ngangali na hawaofii kuunganisha vyama kikubwa wataongeza umakini.


Pia Prof Lipumba amesisitiza kwamba wakati Uchaguzi Mkuu ujao ukiwa umebakisha miezi michache kufanyika ni vizuri uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana ukarudiwa akimiani haukuwa huru na haki.


Ameongeza kuwa tofauti na uchaguzi huo kutaka urudiwe, pia amesisitiza Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike baada ya kufanyika marekebisho ya Sheria na Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na upatikanaji wa Katiba Mpya.


Wakati Prof Lipumba akitoa misimamo hiyo, pia amewaka wazi kuwa kwa sasa kamati ya chama hicho inayoshughulikia uwandaaji wa Ilani ya Uchaguzi inaendelea na mchakato huo kwa kutumia akili Mnemba (AI) ili kupata mawazo mapana ya kusaidia kufikia malengo stahiki.


“Kamati yetu inaandaa ilani ya uchaguzi kwa kutumia akili Mnemba na imani yetu itatatua changamoto mbalimbali zilizopo na kupata ilani iliyobora, pia watanzania wanatakiwa kufahamu kuwa uchaguzi ni gharama, hivyo watuunge mkono kwa lengo la kuleta mabadiliko,” amesema.  

 

No comments:

Post a Comment