KILWA YAENDELEA KUFURIKA WATALII - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Wednesday, March 5, 2025

KILWA YAENDELEA KUFURIKA WATALII


NA BEATUS MAGANJA

MELI ya Kifahari ya kitalii ya "Le Bougainville,"  imewasili leo Machi 05, 2025 katika Hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia Magofu ya Kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara Mkoani Lindi ikiwa na jumla ya watalii 133 kutoka Mataifa mbalimbali duniani Kwa ajili ya shughuli za utalii. Hii ikiwa ni safari  yake ya 7 tangu kuanza kwa msimu wa utalii wa Mwaka 2025


Watalii waliotembelea hifadhi hiyo  wametoka Mataifa ya  Denmark, Australia, Canada, Ufaransa, Marekani, Uingereza na Afrika Kusini huku wengine wakitokea Mataifa ya Uswisi, Romania, Ujerumani, Ubelgiji, New Zealand, na Ireland


Meli hii ya kifahari inahudumia wageni kutoka pande zote za dunia, ikitoa fursa Kwa watalii kutembelea maeneo ya kihistoria na kiutamaduni ya Kilwa, ambayo ni urithi wa dunia wa UNESCO na kuwawezesha watalii  kushuhudia  tamaduni za kiasili zinazopatikana katika hifadhi hii ya kipekee iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA.


Kwa mujibu wa maafisa wa hifadhi hiyo, safari hii ni sehemu ya juhudi za kuendeleza utalii wa kipekee katika mikoa ya Kusini, huku wakisisitiza umuhimu wa utalii endelevu ambao unaleta faida kwa jamii za maeneo husika. Hii ni meli ya saba kuwasili katika hifadhi hiyo tangu kuanza kwa mwaka huu ambayo mpaka kufikia leo imefikisha jumla ya watalii 854  na inatarajiwa kuongeza idadi ya wageni zaidi katika miezi ijayo.


Wageni wamepata fursa ya kujifunza mengi kuhusu historia ya Kilwa, ikiwa ni pamoja na magofu ya Kilwa Kisiwani  maeneo ambayo yalikuwa ya kibiashara na utawala katika zama za utawala wa Kiarabu na Ureno, pia wamepata fursa ya kushirikiana na jamii za wenyeji.


Meneja wa hifadhi ya Kilwa, Mhifadhi Mwandamizi (Malikale) SC Kelvin Stanislaus Fella amesema  "Tuna furaha kuona meli ya "Le Bougainville" ikirudi tena na tena, na kuleta wageni kutoka mataifa mbali mbali. Hii ni fursa kubwa kwa utalii wetu na ni hatua muhimu katika kutangaza Kilwa kama kivutio cha kimataifa."


Meli ya "Le Bougainville" ni miongoni mwa meli za kifahari zinazotumia njia za baharini kutoa huduma za utalii katika maeneo ya Afrika Mashariki huku safari hizi  zikiratibiwa na Kampuni ya Akorn ambayo huwapeleka watalii katika  maeneo mbalimbali duniani  na inatarajiwa kuleta wageni wengi zaidi katika msimu wa utalii wa 2025.






No comments:

Post a Comment