NA MWANDISHI WETU
WAKATI Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo Stadi (VETA) yakiwa katika maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa
kwake, Serikali imekuja na makakati wa kujenga ushirikiano na wadau wengine ili
kuleta tija kwa vijana wanapokuwa vyuoni.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Aldof Mkenda amebainisha hayo leo Machi 5, 2025 jijini Dar es Salaam
wakati akizungumza wa waandishi kuhusu maadhimisho hayo yanayofanyika kuanzia
Machi 8 hadi 21 mwaka huu.
Amesema mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo atakuwa Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa na yatafanyika katika
Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam na kufafanua kwamba yatakuwa ya
kipekee kutokana na taifa kusherehekea mchango madhubuti unaotolewa na VETA
tangu kuanzishwa kwake unaowawezesha vijana kupata ujuzi unaowakwamua kiuchumi.
Amefafanua kwamba kwa sasa mpango
wa Serikali, VETA kujenge ushirikiano wenye viwanda na wadau wengine, mchakato
utakaosaidia vijana wanaojiunga na vyuo hivyo kupata mafunzo ya vitendo kupitia
wadau hao.
Prof Mkenda ametolea mfano uwepo
wa wataalamu mbalimbali wenye uwezo mkubwa wa ubunifu wa kazi zao ambao hawana
elimu ya darasani, mfano mafundi nguo, Seremala, ujenzi ambao wakitumiwa vizuri
wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa taifa.
“Tutawatumia hawa kufundisha wanafunzi
wetu jambo tunaloamini litasadia kuwapa wanafunzi wetu ujuzi wa moja kwa moja
na wakitoa hapo watakuwa wameiva tayari kuingia katika soko la ajira na VETA
kwa kuwatumia hawa mafundi itaondokana na ukosefu wa walimu,” amesema. Huku
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Ukuzaji Stadi na Ubunifu kwa Maendeleo ya
Jamii na Taifa’.
Waziri Mkenda amesema shughuli
mbalimbali zitafanyika katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho hayo,
ikiwemo kutoa huduma kwa jamii, kuendesha maonesho ya teknolojia na ujuzi,
pamoja na kutoa tuzo na vyeti vya heshima kwa watu mbambali kwa mchango wao
katika shughuli za maendeleo ya Ufundi Stadi nchini.
Amesema mwaka huu wataadhimisha
miaka 30 ya VETA ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge mwaka 1994 na kuanza
kazi rasmi mwaka 1995. Kabla ya VETA kulikuwa na Idara ya Mafunzo na Majaribio
ya Ufundi Stadi (NVTD) katika Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii ambayo
ilianzishwa mwaka 1975.
Amesema kwa kipindi cha miongo
mitatu ya VETA imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajengea Watanzania
uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa, na kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi.
Aidha amesema kuwa VETA imekuwa
na mafanikio na kuwa taasisi muhimu inayochangia rasilimali watu yenye ujuzi
inayohudumu katika sekta mbalimbali, ikiwemo Viwanda, Kilimo, Ujenzi,
Teknolojia, Nishati na huduma na Utalii.
“Maadhimisho haya ya miaka 50
ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na miaka 30 ya VETA yanakuja
wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kukamilishwa ujenzi wa vyuo vya
VETA vya hadhi ya kimkoa, katika mikoa yote ambayo haina vyuo hivyo kuanzia
ngazi ya wilaya.
Amesema sasa VETA inakamilisha
ujenzi wa chuo chenye hadhi ya Mkoa cha VETA kwa Mkoa wa Songwe na tunaendelea
na ujenzi wa vyuo 64 katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazina vyuo hivyo.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha
wadau wote katika maadhimisho haya yanayoendelea nchini na upekee katika kilele
cha yatayofanyika jijini Dar es Salaam ili tujionee na kujadili umuhimu wa
elimu na ujuzi kulingana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo yam waka
2014 toleo la 2023,” amesema Profesa Mkenda
No comments:
Post a Comment