IUCN YAWANOA WAANDISHI KUHUSU UCHUMI WA BULUU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, July 24, 2025

IUCN YAWANOA WAANDISHI KUHUSU UCHUMI WA BULUU


NA MWANDISHI WETU, TANGA

MRADI wa Bahari Mali unaotekelezwa na Taasisi ya International Union for Conservation Nature (IUCN), chini ya ufadhilii wa Ubalozi wa Ireland umenufaisha zaidi ya wananchi 400 wa Mkoa wa Tanga na Kisiwa cha Pemba.


Hayo yamesemwa na Meneja wa Miradi ya Uhifadhi wa Habari IUCN  Tanzania, Joseph Olila wakati akizungumza na mwandishi wa habari katika mafunzo kuhusu uchumi wa buluu kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira (JET) yanayofanyika mkoani Tanga.


Olila amesema Mradi wa Bahari Mali umelenga kusaidia shughuli za uchumi wa buluu katika wilaya Mkinga na Pangani mkoani Tanga na Mkoani na Micheweni Kisiwani Pemba.


Amesema katika mradi huo ambao unatatua changamoto zilizopo kwenye uchumi wa buluu,  wanaangalia eneo la uzalishaji, kupitia program ya kusaidia shughuli za kijamii kwenye baadhi ya  mazao ya bahari kama mwani, majongoo habari, unenepeshaji wa kaa na ufugaji wa samaki.


"Lengo la programu hii ni kuwezesha wananchi kujikwamua kwenye umaskini, kufanya shughuli kwa namna endelevu na rafiki kwa mazingira na kuhakikisha uchumi wa buluu unaleta matokeo chanya, jambo ambalo limetokea ,"amesema.


Meneja huyo amesema pia wameweza kuhifadhi na kurejesha baionuwai uoto wa asili eneo la lenye takribani 90.4 mkoani Tanga na Pemba na matarajio yao ni hadi mwisho wa mwaka kufikia hekta 100.


Eneo lingine ni usimamizi ambapo Tanzanian Bara ni Usimamizi wa Fukwe (Beach Management Unit) na Kamati za Uvuvi za Shehia Pemba.


Meneja huyo amesema hadi sasa mradi umewainua wanavijiji kiuchumi, jambo ambalo linawapa faraja wao kama watekelezaji.


Olila amesema pia wameangalia eneo la asidi bahari ambapo wamekuwa wakishirikiana taasisi za kitafiti kupata taarifa sahihi na kuangalia namna ya kuzikabili.


Aidha, Olila amesema jitihada zao zinaendana na utekelezaji Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 katika kuhimiza uchumi wa buluu  kwa kuwataka wananchi kufanya shughuli  endelevu na rafiki kwa mazingira.


Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanznaia (TAFIRI), Dk Rushingisha George amesema wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu Mradi wa Mali Bahari ambapo umeonesha kuwa na matokeo yamekuwa mazuri.


"Sisi TAFIRI kwenye Mradi wa Mali Bahari tumekuwa tukiangalia kipengele cha Asidi Bahari na hali ilionesha bahari yetu imekuwa ikiathirika na tumeweza kutoa taarifa sahihi ambazo zimekuwa zikitumiwa kuidhibiti kwa kutoa elimu na kurejesha hali ya awali," amesema.


Dk Rushingisha amesema Tanzania juhudi zinahitajika kuhakikisha asidi bahari inadhibitiwa na kuifanya bahari iwe endelevu.


Amesema wakiwa wanafanya tafiti wanatarajia matokeo ambayo yatumike kuboresha shughuli zote za uhifadhi.


“Ili kupata matokeo sahihi na chaya  ni vizuri  kuwashirikisha watu ambao wanauwezo wa kuipeleka taarifa kwa wahusika kwa usahihi, waandishi wa habari ni kundi sahihi hivyo ni muhimu wakashirikishwa katika mzunguko mzima wa utekelezaji wa miradi kufikisha taarifa sahihi kwa walaji,” amesema.


Amesema bahari inazidi kuathirika na ongezeko la asidi bahari hivyo kuna mbinu za kukabiliana nazo kwa kupata taarifa sahihi, kufanya tafiti kuangalia athari za tatizo, kutoa elimu na kutekeleza mikakati inayoweza kupunguza athari kwa jamii.


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanachama wake namna ya kuandika habari za uchumi wa bluu na uhifadhi wa mazingira.


Amesema Tanzania inaenda kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo inagusia suala la uchumi wa buluu, hivyo JET imeona ni muhimu sasa kuwajengea uwezo kwenye eneo hilo na uhifadhi kwa ujumla.


"JET kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa elimu kwa wanachama wake kuhusu uhifadhi wa mazingira, hivyo kwa mafunzo haya ya siku nne chini ya IUCN watapatiwa elimu juu ya bahari mali kama nyasibahari, matimbawe na mwani,"amesema.


Chikomo amesema uchumi wa bluu ni nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wanaishi pembezoni mwa bahari.


Amesema JET imekuwa ikijikita kuwafundisha waandishi wa habari kuhusiana na masuala ya hifadhi, misitu, wanyamapori, kuhamasisha utalii nchini.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Dastan Kamanzi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaandaa habari zenye tija kuhusu uchumi wa buluu.


"Mmepatiwa mafunzo kuhusu uchumi wa buluu, naomba muende kuandika habari ambazo zina tija na sio kutoa taarifa, lazima mzingatie uandishi wa kwanini, nini na nani," amesema.


Kamanzi amesema mwandishi lazima aandike habari za kuelimisha, kuwajibisha na kutoanesha matokeo.







No comments:

Post a Comment