NA SOPHIA KINGIMALI
KAIMU Mkurugenzi wa Urekebishaji wa Sheria, Utafiti na Mafunzo, Rehema Katuga ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa huduma bora na muhimu ambazo wanazitoa kwa wananchi, hususani katika kampeni ya muswada wa kisheria ya Mama Samia.
Akizungumza na waandishi wa habari julai 7,2025 katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara amesema Kampeni hii iliyoonyeshwa katika maonesho ya Sabasaba imekuwa na mafanikio makubwa katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wa kawaida.
"Imekuwa fursa nzuri ambapo wananchi wanafika na kupata huduma mbalimbali za msaada wa kisheria. Huduma hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kutatua kero mbalimbali zinazowakumba wananchi katika maisha yao ya kila siku."Amesema
Akizungumzia Ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupitia Ofisi ya Urekebishaji wa Sheria, amesema inashirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha kwamba sheria zinazotekelezwa zinaendana na wakati na zinatoa majibu bora kwa changamoto za kijamii na kisheria.
"Kama Ofisi ya Mwanasheria, tunashirikiana na Wizara katika kuhakikisha kwamba tunawawezesha wananchi kufuata sheria ambazo zina madhumuni ya kutatua migogoro na kuboresha utawala wa sheria nchini," aliongeza.
Katika hatua nyingine, Katuga alisisitiza kuwa, kupitia ushirikiano huu, Wizara ya Katiba na Sheria ilizindua toleo jipya la sheria zilizofanyiwa urekebisho, ikiwa ni pamoja na sheria zote zilizotungwa kuanzia uhuru hadi sasa, pamoja na marekebisho yake.
Marekebisho haya yameweza kutoa suluhisho kwa baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa zinawakumba wananchi. "Wananchi wanapohitaji kuelewa jambo fulani katika sheria, sasa wanaweza kuchukua toleo la sheria ya mwaka 2023 na kupata maelezo yote kuhusu marekebisho yaliyofanywa. Hii inasaidia kwa kuwaelimisha wananchi na kuondoa changamoto za zamani ambapo walilazimika kutafuta sheria za zamani na kuingia katika machafuko ya tafsiri," alifafanua.
Aidha, Katuga alitaja kuwa marekebisho haya yatasaidia kupunguza mifumo ya rushwa na ufinyu wa taarifa, ambapo baadhi ya watu walikuwa hawatoi taarifa za kinaganaga kuhusu mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria. "Hii itasaidia sana katika kutatua migogoro kwa wananchi, kwa sababu sasa wanapata taarifa kwa haraka na kwa usahihi," alisema.
No comments:
Post a Comment