NA MWANDISHI WETU
WATANZANIA wametakiwa kuacha kulalamika na badala yake wametakiwa kutumia katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
“Madai ya Katiba Mpya hayakuanza leo, hivyo CCM haitaweza kujichongea njia ya kujiondoa madarakani kwa maana hiyo madai ya katiba mpya yataendelea kuwepo na hakuna kitakachofanyika kinachotakiwa ni Watanzania kuacha kulalamika, kikubwa tutumie katiba ilipo kuiondoa madarakani (CCM).
“Jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura na mtupigie hadi zimwagike hakika hawataweza kuiba na hiyo ndio itakuwa tiketi ya CCM kuiondoa madarakani mapema tu kwa kutumia katiba hiyo hiyo ambayo hawataki kuifanyia marekebisho”.
Hayo yamebainishwa leo, Agosti 14, mwaka huu na mgombea urais wa Chama Cha Wananchi (CUF), Tanzania Bara, Gombo Samandito wakati mapokezaji yake katika Ofisi za chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam baada ya kurejea kutoka Dodoma kuchukua fomu za uteuzi kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
“Hatuwezi kuilalamikia CCM wakati madaraka ya kuwaondoa tunayo, hakikisheni watanzania siku ya kupiga kura mnatupigia kwa wingi ili kutupa ridhaa kuongoza nchi,” amesema.
Naye mgombea mwenza wa urais Tanzania Zanzibar, Husna Abdallah ametoa wito kwa vijana wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili kuhakikisha CUF inatimiza malengo yake kisiasa.
“Nawaombeni vijana jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilshi na Udiwani ili chama chetu kitimize malengo kisiasa hususan ya kurekebisha katika sheria kandamizi, pindi tutakapoingia kwa wingi katika Baraza la Uwakilishi na Bungeni kila sheria ambayo si rafiki kwa watanzania tutaifanyia marekebisho,” amesema.
Ameongeza kuwa hakuna sehemu nyingine ya kuhakikisha tunarekebisha sheria kandamizi ni kuingia bungeni kwa wingi na hatuwezi kutimiza hayo bila ya wenye sifa kugombea na kupigiwa kura na wananchi na ndio sababu ya kutosusia uchaguzi,” amesema.
No comments:
Post a Comment