WATUMISHI WAHIMIZWA KUJENGA MAKAZI KABLA YA KUSTAAFU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, August 21, 2025

WATUMISHI WAHIMIZWA KUJENGA MAKAZI KABLA YA KUSTAAFU


NA MWANDISHI WETU

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amewahimiza watumishi wa umma kutumia fursa zilizopo katika taasisi za kifedha kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi, ikiwemo kujenga makazi yao binafsi kabla ya kustaafu.


Ushauri huo umetolewa Agosti 20, 2025, wakati Katibu Mkuu huyo alipokutana na wafanyakazi wa wizara hiyo katika kikao cha ndani kilichofanyika jijini Dodoma.


“Tumieni fursa ya mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha nchini ili mjenge maisha yenu mapema. Msisubiri hadi mstaafu ndipo muanze kufikiria kujenga nyumba ya kuishi,” alisisitiza Mhandisi Mramba.


Aidha, alikumbusha watumishi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, weledi, na kuepuka vitendo vya rushwa, sambamba na kutunza mali za serikali kama kompyuta na vifaa vingine vya ofisi.


“Serikali inatumia gharama kubwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kazi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ni wajibu wetu kuvithamini na kuvitumia kwa tija,” aliongeza.


Katika kikao hicho, watumishi walimpongeza Katibu Mkuu kwa utaratibu wake wa kuwa karibu nao kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili, hatua waliyoieleza kuwa imeongeza hamasa na uwajibikaji kazini.


Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Peter, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka wizara hiyo pamoja na watendaji kutoka taasisi mbalimbali za serikali.







No comments:

Post a Comment