DC KASLIDA ATEMBELEA UJENZI WA MADARASA SHULE YA SEKONDARI ASKOFU JOSAPHAT LEBULU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, September 18, 2025

DC KASLIDA ATEMBELEA UJENZI WA MADARASA SHULE YA SEKONDARI ASKOFU JOSAPHAT LEBULU


NA MWANDISHI WETU


MKUU wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, ametembelea mradi wa ujenzi wa madarasa nane ya shule mpya ya sekondari ya Askofu Josaphat Lebulu, mradi unaotekelezwa na Kanisa Katoliki kwa gharama ya shilingi milioni 600.


Katika ziara hiyo, Kasilda amelipongeza Kanisa Katoliki na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha ndoto za kuwahudumia wananchi wilayani Same zinatimia.


Aidha, alibainisha kuwa Kanisa Katoliki limekuwa mshirika muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu ndani ya wilaya kwa kuwekeza shule za msingi nane na sekondari kumi na moja, hatua inayosaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za serikali katika kutoa huduma bora za kijamii.



Kasilda alitumia nafasi hiyo pia kushukuru uongozi wa shule hiyo kwa juhudi za utunzaji wa mazingira, baada ya kupokea na kupanda miche 500 ya miti ambayo kwa sasa inastawi vizuri, huku serikali ikiongeza miche mingine 500 ili kuimarisha kampeni ya upandaji miti wilayani humo (Make Same Green).


Ujenzi wa shule ya sekondari ya Askofu Josaphat Lebulu unatarajiwa kukamilika mwaka 2026 na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2027. Mradi huo utahusisha majengo tisa yenye ghorofa moja, yakiwemo madarasa ya kisasa, mabweni ya wavulana na wasichana, pamoja na ofisi za walimu.


Kwa mujibu wa mpango endelevu, shule hiyo inalenga kutoa elimu kuanzia ngazi ya awali, shule ya msingi, sekondari hadi kidato cha sita. Kwa sasa shule ya msingi chini ya mradi huo inaendelea kutoa huduma tangu mwaka 2017, huku ujenzi wa sekondari ukiendelea kwa kasi.


Hata hivyo, Serikali Wilayani Same imesema inatambua mchango wa taasisi za dini na imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi na mashirika ya Dini ambayo yamekuwa yakitoa huduma mbalimbali za kijamii wilayani humo kwa kuhakikisha wanawekewa mazingira wezeshi ili wananchi waendelee kupata huduma bora.


No comments:

Post a Comment