DKT. SAMIA ALIVYOFUTA KILIO CHA TOZO KANDAMIZI MIKOPO ELIMU YA JUU - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, October 23, 2025

DKT. SAMIA ALIVYOFUTA KILIO CHA TOZO KANDAMIZI MIKOPO ELIMU YA JUU


NA MWANDISHI WETU

UNAPOZUNGUMZIA Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), si jina geni kwa Watanzania na hata kimataifa.


Hadi kufikia sasa ikiwa na miaka 21 tangu kuanzishwa kwake, taasisi hii imekuwa mhimili muhimu katika kufanikisha ndoto za maelfu ya vijana kupata elimu ya juu nchini.




Hata hivyo, safari yake haijakosa misukosuko. Miaka minne iliyopita, HESLB ilijikuta katikati ya mjadala mzito wa kitaifa uliohusisha lawama, mapendekezo na wito wa mageuzi katika namna inavyotoa huduma, inavyokusanya madeni na jinsi inavyowajibika kwa walengwa wake. 


Mjadala huo ulisababisha serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mapitio makubwa yaliyolenga kuboresha taasisi hiyo kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi. 


ASILI YA HESLB


Bodi hii ilianzishwa kwa sheria mwaka 2004, ikiwa na jukumu la kutoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye uwezo mdogo kifedha, pamoja na kukusanya marejesho ya mikopo hiyo.


Ingawa bodi hii ilianzishwa mwaka huo, mfumo wa mikopo kwa wanafunzi ulianza tangu mwaka 1994, miaka 31 iliyopita, kwa lengo la kusaidia watoto wa familia zisizo na uwezo mkubwa kiuchumi.



Awali, serikali ilikuwa ikigharamia sehemu kubwa ya ada na mahitaji ya wanafunzi, lakini kadri miaka ilivyopita, mzigo wa gharama ulihamia zaidi kwa wanafunzi, huku mifumo ya marejesho ikiwa haijawekwa wazi. Hapo ndipo HESLB ilipopewa nguvu za kisheria kusimamia jukumu hilo kwa uwazi zaidi.


DOSARI ZILIZOGUNDULIWA


Ukaguzi maalum wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, uliowasilishwa kwa Rais Samia Machi 2021, uliweka wazi changamoto nzito ndani ya HESLB.


Ripoti hiyo ilibainisha ucheleweshaji utoaji mikopo, udhaifu katika ukusanyaji madeni na utegemezi mkubwa kwa serikali, takribani asilimia 66 ya bajeti yake.


CAG alionya kwamba mwenendo huo ulihatarisha uhai wa HESLB na mustakabali wa wanafunzi wapya. Kwa mujibu wa ripoti yake, idadi ya wadaiwa sugu iliongezeka kwa kasi, kutoka 163,394 mwaka 2015/16 hadi 291,672 mwaka uliofuata, sawa na ongezeko la zaidi ya watu 128,000. 



Zaidi, kati ya Sh. trilioni 2.4 ambazo zilipaswa kukusanywa kwa kipindi cha miaka mitano (2012/13–2016/17), bodi ilifanikiwa kukusanya Sh. bilioni 221 pekee. Hali hiyo, kwa mujibu wa CAG, iliashiria hatari kubwa kwa uendelevu wa huduma hiyo muhimu kwa vijana wa kitanzania.


Ukaguzi mwingine wa CAG katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ulibaini “uonevu wa makato” unaotokana na mikopo ya HESLB. Baadhi ya watumishi walikatwa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa kisheria, hivyo kupokea chini ya theluthi moja ya mshahara wao.


Katika mamlaka 35 zilizokaguliwa, watumishi 3,038 walibainika kuwa waathirika wa makato hayo makubwa.


CAG alibainisha kuwa kasoro hujitokeza pale mdaiwa wa bodi anaporuhusiwa kuchukua mikopo mingine yenye makato yanayomfanya kukiuka alipwe chini ya theluthi moja ya mshahara, huku katika baadhi ya halmashauri kukibainika kuwapo watumishi wasiolipwa kitu kutokana na mikopo inayowakabili.



Alitaja baadhi ya halmashauri na idadi ya waathirika wake katika mabano, wasioambulia chochote katika mishahata yao, ni Jiji la Arusha (1), wilaya za Kiteto (1), Rombo (3) na Same (1) pamoja na Manispaa ya Temeke (1) na Mji Njombe (1).


“Ninapata wasiwasi na ustawi wa watumishi hawa katika kupata mahitaji yao muhimu kama vile chakula, mavazi na malazi.


“Hali hii inawaweka watumishi katika mazingira magumu ya maisha, na wengine hulazimika kufanya shughuli binafsi wakati wa kazi ili kujiongezea kipato,” alisema CAG Kichere.


Ni hali inayokinzana na Kifungu cha 3 cha Sheria ya Maofisa Waliobainishwa (Urejeshwaji Madeni), Sheria Na. 7 ya Mwaka 1970 na Mwongozo wa Serikali wenye Kumbukumbu Namba 26/46/01/1/66 wa Novemba 28,2012. Vyote hivi vimeweka masharti kwamba “watumishi wanapaswa kulipwa si chini ya theluthi moja ya mishahara yao ya kila mwezi”.



SAUTI YA BUNGE


Bunge nalo halikusalia kimya. Aliyekuwa Spika wake, Job Ndugai, alionya kuwa utendaji wa HESLB unahatarisha ndoto za watoto wa masikini. Alikosoa tozo ya asilimia sita iliyokuwa ikiwekwa kila mwaka kwa jina la “kutunza thamani ya mkopo,” akisema ni mzigo kwa wanufaika. 


“Huwezi kumwambia mtoto wa masikini kwamba unamkopesha elimu kisha unamtoza riba. Hii si msaada bali biashara,” alisema. 


Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko (CHADEMA), alienda mbali zaidi, akidai sheria inayounda HESLB ni kandamizi. Alitaja makato ya asilimia 15 kwenye mishahara, pamoja na adhabu ya asilimia 10 kwa kuchelewa kulipa mwaka mmoja baada ya kuhitimu, kuwa ni vikwazo vinavyomdhoofisha mnufaika.


“Huu mkopo unapaswa kumsaidia mtoto wa masikini, si kumzidishia mateso,” alisema Matiko, akiahidi kuwasilisha muswada binafsi wa marekebisho ya sheria hiyo.



Huku akitafsiri kinachofanywa na bodi hiyo kwamba ni “uonevu”, Esther – Mhadhiri wa zamani wa Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alishauri:


“Serikali ifanye marejeo ya sheria hii ya mikopo ya elimu ya juu. Makato ya asilimia 15 ya mshahara wa mwajiriwa ni makubwa mno, ukizingatia huyu mtu anakatwa makato mengine ikiwamo PAYE (Kodi ya Mshahara), bima ya afya na makato mengineyo.


“Hata hiyo penati ya asilimia 10 kama akishindwa kuanza kulipa mkopo baada ya mwaka mmoja tangu ahitimu masomo, ni tatizo. Hii ni sheria kandamizi.”


SAMIA AINGILIA KATI


Rais Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake ya Mei Mosi 2021, alisikiliza kilio hicho. Alitangaza kufuta tozo ya asilimia sita kwa mwaka ambayo ilikuwa ikiongeza mzigo kwa wanufaika. 


Siku tatu baadaye, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alitangaza kufutwa kwa adhabu ya asilimia 10 kwa waliochelewa kuanza kulipa. 


Serikali pia iliahidi kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji madeni na huduma kwa wateja. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, Sh. bilioni 570 zilitengwa kuwasaidia wanafunzi 168,000 wa elimu ya juu.


RIBA ILIUMIZA


Mnamo Agosti 6, 2019, mwandishi wa makala hii alizungumza na Meneja wa Habari wa HESLB, Omega Ngole, alikiri kuwa tozo ya asilimia sita kila mwaka ilisababisha wanufaika wengi kushindwa kulipa madeni yao. 

"Hivyo Dkt Samia kuiondoa ni jambo la kumpongeza na kumtakia maisha marefu yenye mwisho mwema.







No comments:

Post a Comment