NA MWANDISHI WETU, NGARA KAGERA
WAKATI kampeni za Uchaguzi Mkuu zikizidi kushika kasi, mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan, ameahidi kujenga Hospitali ya Kanda na soko la kisasa katika Mkoa wa Kagera, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha huduma za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi.
Akihutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ngara, Doyo alisema hospitali hiyo itakuwa na vifaa vya kisasa na wataalamu wa afya ili kuhakikisha wananchi wa Kagera wanapata huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
“Sekta ya afya imesahaulika kwa muda mrefu, ilhali afya ndiyo uti wa mgongo wa taifa. Taifa lisilo na wananchi wenye uhakika wa huduma za afya ni taifa dhaifu linalopoteza nguvu kazi kila mwaka. Ndiyo maana dhamira yangu ni kuwekeza kikamilifu katika sekta ya afya,” alisema Doyo.
Aidha, Doyo aliahidi kujenga soko la kisasa la mazao litakalowawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei nzuri, kuongeza thamani, na kuimarisha uchumi wa mkoa huo unaotegemea kilimo. Pia aliahidi kuboresha zao la kahawa, kwa kuhakikisha linapata thamani stahiki sokoni.
Mbali na hilo Doyo, alisisitiza mpango wa kufungua fursa za kibiashara kwa kujenga Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kununua ndege ya mizigo kwa ajili ya kusafirisha mazao ya kilimo, hususan ndizi, kahawa na mazao mengine yanayozalishwa kwa wingi Kagera, kwenda Dar es Salaam na nchi jirani.
“Katika ukuaji wa uchumi ni lazima Kagera ipate reli ya kisasa (SGR) na ndege kubwa ya mizigo. Mazao ya wakulima yatasafirishwa kwa haraka na kufika sokoni bila kuchelewa, hata katika nchi jirani kama Burundi, Rwanda na Uganda,” aliongeza Doyo.
Kwa upande wake, Hadija Dikulumbale, mmoja wa wahamasishaji wa kampeni hizo, alisema chama hicho kimedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara za Kagera. Alifafanua kuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Ngara na maeneo ya mpakani ni barabara mbovu, jambo linalokwamisha usafirishaji wa mazao sokoni.
“Barabara bora ndiyo msingi wa maendeleo. Zikitengenezwa kwa ubora, zitawawezesha wakulima kufikisha mazao yao popote, ndani ya mikoa jirani na hata nje ya nchi,” alisema Dikulumbale.
Naye, Zaidat Fundi Majiamoto, Mwenyekiti wa Kigoda cha Kina Mama Taifa kupitia chama hicho, alisisitiza kuwa wanawake wengi wanapitia changamoto kubwa wakati wa kujifungua kutokana na upungufu wa dawa na vifaa hospitalini.
“Kina mama wa Kagera wamekuwa wakikosa amani wakati wa kujifungua, wakilazimika kwenda hospitali na vifaa vyao wenyewe. Hii si haki. NLD, tunaamini Doyo atakomesha changamoto hii kwa kujenga hospitali kubwa ya kanda na kuhakikisha dawa zinapatikana,” alisema Majiamoto.
Majiamoto aliongeza kuwa Mkoa wa Kagera umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo huduma hafifu za afya, barabara zisizo na viwango, masoko duni ya mazao ya kilimo kama cha kahawa, pamoja na changamoto za kibiashara kutokana na mazingira ya mpakani. Alisisitiza kuwa ahadi za mgombea huyo wa NLD zimebeba matumaini mapya kwa wananchi wa Ngara na mkoa mzima wa Kagera kwa kuwa zinatokana na ilani yenye tafiti makini na maono ya mabadiliko.
Msafara wa kampeni za mgombea urais huyo wa NLD unaelekea mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida kuendelea na mikutano ya kampeni.
No comments:
Post a Comment