DOYO AAHIDI MAPINDUZI YA ELIMU, AJIRA NA MIUNDOMBINU MOROGORO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, October 9, 2025

DOYO AAHIDI MAPINDUZI YA ELIMU, AJIRA NA MIUNDOMBINU MOROGORO


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

MGOMBEA urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, akiendelea na kampeni zake mkoani Morogoro, amesema chama chake kimejipanga kwa dhati kuwakomboa vijana wa Kitanzania kupitia elimu bora itakayokuwa suluhisho la changamoto za ajira na utegemezi.


 Doyo amesema kuwa mfumo wa sasa wa elimu umekuwa ukizalisha vijana wanaomaliza vyuo vikuu bila uwezo wa kujitegemea au kubuni miradi ya maendeleo. Kupitia Ilani ya Uchaguzi ya NLD 2025–2030, chama hicho kitaleta mageuzi makubwa katika mtaala wa elimu kwa kuzingatia elimu ya vitendo badala ya ile ya kukariri.



“Elimu tuliyonayo sasa haina tija. Kijana wa Kitanzania anamaliza chuo kikuu lakini hawezi kubuni chochote cha kumsaidia kujitegemea. Sisi NLD tumejipanga kubadili hili. Tutaanza na elimu ya vitendo, kisha kutoa mikopo isiyo na riba kwa wahitimu ili waanzishe miradi yao,” alisema Doyo.


Amefafanua kuwa mikopo hiyo isiyo na riba itasaidia vijana waliopata elimu ya vitendo na ufundi kuwa kichocheo cha ubunifu na uzalishaji, huku ikijumuisha elimu ya ujasiriamali na ulipaji kodi kwa hiari. “Kijana atakayepata mkopo huu ataurejesha kwa njia ya ulipaji kodi, si kwa masharti magumu. Hii itamjengea moyo wa uzalendo katika taifa lake na kumfanya ajitume zaidi,” alisisitiza Doyo.


Aidha, Mhe. Doyo amepongeza Mkoa wa Morogoro kwa historia yake ya kutoa vipaji vingi katika sekta mbalimbali za michezo tangu miaka ya 1970 na 1980. Amesema Chama cha NLD kitaiendeleza historia hiyo kwa kuwekeza katika michezo kama nyenzo ya ajira na maendeleo ya taifa.


Ameahidi kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali yake itajenga viwanja vitano vya kisasa vya michezo mkoani Morogoro kama sehemu ya mpango wa kukuza vipaji na uchumi wa vijana wa mkoa huo,  Amesema mkoa huo unaotoa vipaji vingi vya soka. Amewataka vijana kutumia vipaji vyao kama ajira mbadala badala ya kusubiri ajira za serikali.


Mhe. Doyo pia ameahidi kujenga Barabara Kuu ya Morogoro Road kwa kiwango cha kisasa, ikiwa na barabara mbili kila upande, ili kuondoa msongamano na kupunguza ajali za mara kwa mara katika barabara hiyo.


Kwa upande wake, Mzee Toz Matwanga, Mwenyekiti wa Kigoda cha Wazee wa NLD, aliwaambia wananchi wa Morogoro:

“Michezo si burudani pekee kama ilivyokuwa miaka ya 1960, bali ni ajira mbadala kwa kizazi cha sasa na kijacho. Wananchi wa Morogoro, mchagueni Mhe. Doyo ili alete ubunifu wa ulipaji kodi kwa hiari kupitia mikopo isiyo na riba, na kuunda fursa zitakazowawezesha vijana kujitegemea.”


Msafara wa kampeni wa Chama cha NLD unaelekea mikoa ya Mbeya na Rukwa kuendelea na mikutano ya hadhara, huku kuibua hoja, na sera zinazohimiza ubunifu na maendeleo ya vijana.

No comments:

Post a Comment