NA MWANDISHI WETU
SHUGHULI za madini katika Mkoa wa kimadini Chunya mkoani Mbeya zimechangia ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa kisasa wilayani humo, kupitia michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wa madini.
Akizungumza katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary kutoka Wizara ya Madini, Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Ujenzi wa Uwanja huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa KenGold Sports Club, Keneth Mwakyusa amesema kuwa, kujengwa kwa uwanja huo kunatokana na jitihada zilizofanywa na Halmashauri ya Chunya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa sekta ya madini.
"Tunaweza kusema mapato ya madini pia yamehusika katika ujenzi wa uwanja kwa sababu wadau waliochangia wapo pia wa madini ambao wametumia fedha zilizotokana na na shughuli za madini lakini wapo na wadau wengine nje ya madini na usimamizi mkuu umefanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chunya akisaidiana na kamati ya ujenzi,’’ amesema.
Ameongeza kwamba, uwanja huo utatumiwa na timu za Chunya ikiwemo KenGold na siku za usoni wanatarajia timu kubwa za Yanga, Simba, Azam na nyingine .
Amesema uwepo wake ukitarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kama hoteli, usafiri, chakula na nyingine na kuongeza kwamba hatua iliyofikiwa hivi sasa ni uwekaji wa nyasi bandia.
Akizungumzia mwenendo wa timu ya Kengold amesema timu hiyo inaendelea na mazoezi na wana imani itarejea ligi kuu kwenye msimu ujao na kuwataka wadau wa michezo nchini wakiwemo wananchi wa Chunya kuendelea kuiunga mkono timu hiyo.
Naye, Fundi wa uwanja huo Msafiri Napanja amesema kazi inayoendelea hivi sasa ni uwekaji wa nyasi bandia iliyopangwa kufanyika ndani ya siku 30 huku maendeleo ya ujenzi wa uwanja yamefikia asilimia 85.
Awali, akizungumza na timu hiyo ya Madini Diary, Afisa Madini Mkoa wa Kimadini Chunya Mhandisi Laurent Mayalla amesema kwamba mchango wa sekta ya madini wilayani Chunya umeyagusa maeneo mengi ikiwemo ya michezo kutokana na ujenzi wa uwanja huo.









No comments:
Post a Comment