NEEC YAWANOA WAANDISHI DAR - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, October 10, 2025

NEEC YAWANOA WAANDISHI DAR


NA MWANDISHI WETU

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limewajengea uwezo Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar Salaam ili waandike taarifa zinazohusu baraza hilo kwa usahihi  na kuwafikia wananchi kwa upana na uelewa chanya.

Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Neema Mwakatobe, akifungua mafunzo hayo leo jijini Dar es Salaam amefafanua kwamba Waandishi wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu NEEC watasaidia kuwafahamisha wananchi namna wanavyoratibu shughuli za uwezeshaji kiuchumi pamoja na fursa zinazotolewa katika kushiriki kwenye shughuli kiuchumi.

“Ni muhimu kwa wananchi kufahamu wapi pa kwenda wanapokutana na changamoto, fursa zilizopo za uwezeshaji, na sababu za uwepo wa Baraza hili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaendeleo,” amesema Mwakatobe.

Mwakatobe ameongeza kuwa NEEC ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, na jukumu lake kuu ni kufuatilia na kutathmini shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini. 

Alifafanua kuwa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilianzishwa mwaka 2004, ikifuatiwa na Sheria ya mwaka 2005 iliyoanzisha rasmi Baraza hilo kwa madhumuni ya kuratibu, kufuatilia na kuhakikisha wananchi wanashiriki ipasavyo katika shughuli za kiuchumi.

Ameongeza kuwa Baraza hufanya kazi kwa karibu na wizara, taasisi na wadau mbalimbali wenye programu na bajeti za kuwawezesha wananchi, na hufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa kikamilifu.

Aidha, alisema ni wajibu wa NEEC kufahamu wadau wote wanaotekeleza shughuli za uwezeshaji na kutoa taarifa kwa umma kuhusu fursa zilizopo, ili wananchi wapate taarifa sahihi za uwezeshaji.

Pia Katibu wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), Selemani Msuya, alishauri mafunzo hayo yawe endelevu ili kuwapa wanahabari mabadiliko mbalimbali kuhusu shughuli za Baraza hilo.

“Tunaishukuru NEEC kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari. Kupitia semina hii, wanachama wetu watakuwa mabalozi wazuri wa kufikisha taarifa za uwezeshaji kwa wananchi,” alisema Msuya.

Aliongeza kuwa JOWUTA kwa sasa ina wanachama zaidi ya 500 nchini, wakiwemo zaidi ya 150 kutoka mkoa wa Dar es Salaam, na aliomba NEEC kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari wa mikoa mingine ili kuendelea kuelimisha umma kwa usahihi.

Naye, Gwakisa Bapala ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa NEEC,  amesema bado wananchi wanatakiwa kupata elimu na changamoto kubwa ni baadhi ya watanzania kutojitambua kwenye kazi.

"Kuna wajibu wa Waandishi wa Habari kusambaza taarifa Kwa kina ili wananchi waweze kuzifahamu fursa za kichumi, pia kutokana na baadhi  ya wananchi kutojitambua itafanya baadhi ya waajiri kufikilia kuomba kibari serikalini ili kuajiri watu kutoka nje ya nchi," amesema.






No comments:

Post a Comment