MACHIFU 200 KANDA KUSINI KUPEWA SEMINA YA UONGOZI, MALEZI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Sunday, October 5, 2025

MACHIFU 200 KANDA KUSINI KUPEWA SEMINA YA UONGOZI, MALEZI


NA MWANDISHI WETU

SHIRIKA la Akida Wabu Development Foundation (AWADEF), Umoja wa Machifu na Serikali wanatarajia kutoa mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo zaidi ya Machifu 220 kutoka mikoa ya Kusini mwa Tanzania.


Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa AWADEF, Chifu Saad Wabu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya ambapo ameitaja mikoa ambayo machifu wake watapata mafunzo kuwa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Morogoro, Mbeya, Songwe na Rukwa.


Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Oktoba 9 hadi 12 na kushirikisha washiriki 220 kutoka mikoa hiyo pamoja na waalikwa wengine ambao ni taasisi za umma na binafsi. 


"Malengo ya semina hiyo ni kukuza uelewa wa machifu katika masuala mbalimbali ikiwemo uongozi, ulinzi wa mtoto, sayansi ya malezi na makuzi, itifaki, uzalendo na uelewa wao wa mifuko ya dhamana ya uwekezaji na bima ya afya.


Pia kutakuwa na mada mbalimbali zitakazotolewa na wataalamu kutoka UNICEF, TECDEN, Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mahakama ya Tanzania na mashirika mengine ambayo yamejitokeza kutoa mafunzo," amesema.


Amesema semina hiyo imeandaliwa kipindi muafaka kutokana na mabadiliko yanayojitokeza pamoja na kuwafanya machifu kuendana na nyakati kwa kuzingatia mazingira tuliyonayo. 


Mwenyekiti huyo amesema dunia sasa inaenda na wakati, hivyo AWADEF ikaona ni muhimu kuandaa semina hii ambayo tunaamini itasaidia kuongeza maarifa mapya kwa machifu wa mikoa hii ya Kusini.  Kauli mbiu yetu kwenye semina hii “ Uongozi wa kimila kwa Amani, Uwajibikaji, na Maendeleo Endelevu”.


Aidha, Wabu amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Mgeni maalum Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana.


Pia kwa namna ya pekee tunamtarajia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete atakuwa miongoni mwa watoa mada kuhusu historia za uchifu na machifu Tanzania.


Chifu Wabu amesema semina hiyo inatarajiwa kufungwa na Kiongozi Mkuu wa Machifu Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan (Chifu Hangaya).


Kwa upande mwingine Chifu Wabu ameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iendelee kushirikiana nao katika kukamilisha maandalizi ya semina hiyo muhimu.


 

Pia tunaomba kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali taasisi za umma, binafsi, makampuni, wizara na idara nyingine kutusaidia kufanikisha semina hii pamoja na matembezi ya amani.

No comments:

Post a Comment