Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, akizungumza wakati akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Utatu Mtakatifu Masakta, Jimbo Katoliki la Mbulu, wilayani Hanang’ mkoani Manyara Desemba 28, 2025.
Na Dotto Mwaibale
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, Mungu ameendelea kumpa kibali
cha kuongoza harambee za uchangiaji wa shughuli za kidini ambazo zimekuwa na
mafanikio makubwa.
Desemba 28, 2025 Mhe. Sillo aliongoza harambee ya kuchangia
ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Utatu Mtakatifu Masakta, Jimbo Katoliki la
Mbulu, wilayani Hanang’ mkoani Manyara ambapo jumla ya Sh.Milioni 37
zilipatikana.
Harambee hiyo inakuwa ya pili kuifanya tangu
alipochaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
baada ya ile aliyoifanya Novemba 23, 2025 katika Kanisa la Tirano lililopo eneo la Galapo mkoani
humo ambapo alichangisha Sh. Milioni 5.7 kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya
muziki ambavyo vitatumika kuhubiri injili kwa njia ya uimbaji.
Jambo
hilo katika imani siyo dogo linaonesha ni jinsi gani Mungu anavyompa kibali
mtumishi wake huyo katika kufanya kazi yake ya kuwatumikia
wananchi kwa namna tofauti.
Katika
harambee zote hizo Mhe. Sillo amekuwa akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika
shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na ujenzi wa nyumba za ibada.
Aidha, jambo lingine ambalo amekuwa akilihimiza ni Watanzania
kuendelea kuilinda na kudumisha amani na kueleza kuwa amani ndiyo inayowafanya
watu waweze kukutana na kufanya shughuli za maendeleo na kuabudu ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba
viongozi wa dini kuendelea kumuombea Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakiwemo
wabunge.
Akizungumza katika harambee hiyo Paroko wa Parokia ya Utatu
Mtakatifu Masakta, Padre Gabriel Mrina, alimshukuru Naibu Spika kwa kuitikia
wito wa kuongoza tukio hilo la Baraka na kumtakia mafanikio zaidi katika
kulitumikia Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia, Karoli Paulo, alisema
kanisa hilo litaendelea kuhubiri amani amani na kuwakumbusha waumini wake kuendelea
kuwa na maadili mema, upendo na kuheshimiana pasipo kumbagua mtu.
Katika harambee hiyo iliyohusisha michango ya waumini na
wadau mbalimbali, jumla ya Sh. Milioni 37 zimepatikana na kiasi cha fedha
zinazohitaji ili kukamilisha ujenzi huo ni Sh. Milioni 49.
Kanisa hilo lenye vigango saba, chini ya Mapadri wa Shirika
la Utume wa Yesu, lilianza mwaka 2001 na limekuwa kitovu muhimu cha ibada na
huduma za kijamii kwa waumini wa eneo la Masakta.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, akiwemo Paul Andrew alisema kukamilika kwa ujenzi wa kanisa hilo kutakuwa na tija kubwa kwa wananchi wa eneo hilo la Masakta na wilaya ya Hanang’ kwa ujumla.
Viongozi wa kanisa hilo wakiwa kwenye harambee hiyo.
Muonekano wa kanisa hilo ambalo ujenzi wake unaendelea.
Credit, WH- NEWS







No comments:
Post a Comment