NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za michezo na uongozi wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza usawa na maendeleo ya sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa leo na Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, kupitia kituo cha redio cha EFM na kusisitiza umuhimu wa kutambua na kuenzi mchango wa wanawake kwenye sekta ya michezo nchini.
Msitha ameeleza kuwa wanawake wamekuwa na nafasi kubwa katika kukuza na kuendeleza michezo nchini kupitia ushiriki wao kama wanamichezo, viongozi wa vyama na vilabu, pamoja na wadau mbalimbali wanaosaidia maendeleo ya michezo.
Kuhusu maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, Msitha amesema Tanzania kwa kushirikiana na nchi washirika inaendelea kufanya maandalizi mbalimbali ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa.
Amesisitiza kuwa maandalizi hayo yanahusisha maboresho ya miundombinu ya michezo, kuimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali pamoja na kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika kufanikisha mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Msitha ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini na kuthamini mchango wa wanawake ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.





No comments:
Post a Comment