BRELA YAIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA KWA KUTOA HUDUMA SAIDIZI KWA WAMILIKI VIWANDA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, March 28, 2026

BRELA YAIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA KWA KUTOA HUDUMA SAIDIZI KWA WAMILIKI VIWANDA


NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa huduma saidizi kwa wamiliki wa viwanda jijini Dar es Salaam kwa kuwasaidia kuhuisha leseni zilizoisha muda wake, kusajili viwanda vilivyokuwa havina leseni pamoja na viwanda visivyokuwa na leseni ya biashara.


Utoaji wa huduma hizo umefanyika, Machi 26, 2026 ikiwa ni muendelezo wa zoezi la ukaguzi elimishi viwandani linalofanywa na BRELA jijini humo ikilenga kuwasaidia kutatua changamoto zao, kupata takwimu halisi za viwanda na kuweka mazingira wezeshi ya biashara kwa wawekezaji.


Akizungumza wakati wa utoaji huduma hizo, Afisa Leseni kutoka BRELA, Koyan Abubakar alisema ukaguzi huo umelenga kutoa elimu na msaada wa kitaalamu kwa wamiliki wa viwanda ili waweze kuendesha biashara zilizorasimishwa kwa ufanisi zaidi.


“Bado tunaendelea na ukaguzi elimishi kwenye viwanda hapa Dar es Salaam, tunataka kuona viwanda vinafanya kazi katika mfumo rasmi, vinazingatia sheria na vinachangia katika ukuaji wa uchumi hapa nchini,” alisema Bw. Koyan.


Nao baadhi ya wamiliki wa viwanda waliofikiwa na huduma hizo walieleza kuridhishwa na juhudi za BRELA za kuwa karibu zaidi na wawekezaji, wakisema kuwa hatua hiyo imewasaidia kuelewa vyema taratibu za leseni na kuwapa urahisi wa kuendesha shughuli zao kisheria.


“Kwa mfano mimi, nilikuwa natuma maombi lakini nakosea, kwa mtu mwingine ambaye anataka kuhuisha leseni yake na anapitia changamoto asiache kuwasiliana na BRELA kwa kuwapigia simu kuomba msaada kwa sababu wanaweza kukusaidia kama nilivyosaidiwa mimi,” alisema Mariam Kigula, Meneja wa kiwanda cha Leading East Africa Ltd.


Ukaguzi elimishi unaofanywa na BRELA katika maeneo ya viwanda jijini Dar es Salaam unatarajiwa pia kufanyika katika mkoa wa Pwani ikiwa ni utaratibu wa taasisi kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji,  wafanyabiashara pamoja na kukuza uchumi wa viwanda nchini.




No comments:

Post a Comment