NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amewaelekeza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuzisimamia Halmashauri zao kuhakikisha zinaweka siku maalum ya kusikiliza malalamiko na kero za wananchi katika ngazi ya kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na ufumbuzi wa changamoto kwa wananchi wa ngazi ya chini.
Maelekezo hayo ameyatoa Machi 2, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara unaofanyika katika Ukumbi wa Lush Garden Hotel jijini Arusha, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Timu ya Usimamizi wa Halmashauri (CMT) kuwa karibu na wananchi na kusikiliza kero zao mapema badala ya kusubiri ziibuliwe wakati wa ziara za viongozi wakuu wa kitaifa.
Amesema kukosekana kwa utaratibu wa kuwasikiliza wananchi katika ngazi ya halmashauri kumesababisha wananchi wengi kujitokeza na malalamiko wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa, hususan ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, inayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha, Prof. Shemdoe amewaelekeza Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kusimamia kikamilifu changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii, akisisitiza kuwa mwalimu ni kioo cha jamii na ana jukumu la kutoa malezi na mafundisho yatakayojenga maadili mema kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha ukuaji wa kasi wa sayansi na teknolojia, walimu wanapaswa kuwafundisha wanafunzi matumizi sahihi ya TEHAMA, hususan katika mitandao ya kijamii, ili teknolojia iwe chachu ya kuimarisha maadili na si kuyadhoofisha.
Wakati huo huo, Prof. Shemdoe amewasisitiza Maafisa hao kuhakikisha kuwa wanafuatilia kwq karibu na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ya kuhakikisha ndani ya miezi sita kila shule nchini kunakuwa na vyoo vya kutosha vya wanafunzi na walimu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Atupele Mwambene, amesema Mkutano Mkuu huo wa 12 umebeba kaulimbiu isemayo “Matumizi ya TEHAMA ni Nguzo Muhimu ya Uboreshaji wa Elimu Tanzania” na unalenga kufanya
majadiliano yenye tija yatakayoboresha na kuimarisha sekta ya elimu nchini.








No comments:
Post a Comment