DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 1,983 ZA DAWA KULEVYA, DIWANI NA WENZAKE 77 MBARONI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, April 13, 2026

DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 1,983 ZA DAWA KULEVYA, DIWANI NA WENZAKE 77 MBARONI


NA MWANDISHI WETU


MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika Operation ya mwezi Machi imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31. 


Hayo yamebainishwa leo na Kamishna wa DCEA, Aretas Lymo   na kubainisha kwamba dawa zilizokamatwa ni za dawa mbalimbali za kulevya ikiwemo kilogramu 3,012.5 na lita 

17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya ku


Pia amesema kwamba ukamataji huo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana 

na makosa hayo.


Aidha amefafanua kwamba  katika matukio hayo, magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa na kutokana na uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo 

kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo. 


"Hali hii imetokana na 

mkakati wa Mamlaka kujikita katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani, "amesema


Amesema baadhi ya matukio ya ukamataji yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini ni ikiwemo Dar es Salaam, katika eneo la Tegeta Kibo ambapo kilogramu 101.2 za mirungi zilikamatwa zikiwa zimefichwa 

katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ lililokuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania. Dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali 

ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika.


Ameongeza kuwa  watuhumiwa 

waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi hilo Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta, 

Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39). Mkoani Pwani kilogramu 419.09 za 

mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam.


Katika Mkoa wa Mwanza, zilikamatwa kilogramu 52 za mirungi katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na 

Bandari ya Mwanza South, ikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso yenye namba ya usajili T 296 APA.


Amefafanua kwamba dawa hizo zilikuwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine, ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba. Dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana alikamatwa.


Aidha, wilayani Misungwi mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa 

Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55). Dawa hizo zilibainika ndani ya nyumba na katika vyombo 

vya usafiri ambavyo ni Gari aina ya Toyota Crown yenye namba ya usajili T 742 EGL, Toyota Wish yenye namba ya usajili T 854 DXB, pamoja na bajaji yenye namba za usajili MC 261 EZV. 


Pia katika mkoa Tanga, zilikamatwa Kilogramu 32.95 za Mirungi ikiwa imefichwa ndani ya mfuko kwa kuchanganywa na 

maembe. Katika tukio hilo, Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao, mkazi wa Mtaa wa Taifa Barabara ya 

13, ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa alikamatwa. Katika operesheni nyingine zilizofanyika mkoani 

humo, jumla ya Kilogramu 164.01 za Mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti. 

Vilevile, mkoani Arusha, katika wilaya ya Longido, Kilogramu 106.25 za Mirungi zilikamatwa zikiwa 

zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish yenye namba ya usajili T 889 DPG. Katika tukio hilo, watuhumiwa 

Solomon Koholo (38), Diwani wa Kata ya Kimokouwa pamoja na Lekaneti Kukuu (38) walikamatwa. Aidha, 

Kilogramu 138.42 za dawa za mirungi zilikamatwa katika matukio mengine yaliyofanyika mkoani humo.

Kadhalika mkoani Kilimanjaro, katika eneo la Himo na Same, Kilogramu 68.3 za mirungi zilizowahusisha

watuhumiwa Amin Mazua (58) maarufu kwa jina la Mbaruku na Wilbard Mchau (50).

Sambamba na udhibiti wa mirungi, aina nyingine ya dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali 

nchini. 


Katika jiji Dar es Salaam, kwenye hosteli ya wanafunzi iliyopo mtaa wa Nzasa, Kijitonyama zilikamatwa Paketi 141

za bangi aina ya skanka. Katika tukio hilo, alikamatwa mtuhumiwa Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli 

hiyo ambaye dawa hizo zilipatikana ndani ya chumba chake katika hosteli hiyo. Tukio hili linaashiria uwepo wa 

mienendo ya biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yanayozunguka taasisi za elimu. Mamlaka inatoa 

wito kwa jamii, hususani wamiliki na wasimamizi wa makazi ya wanafunzi, kushirikiana na vyombo vya dola 

kuhakikisha mazingira ya wanafunzi yanabaki salama bila dawa za kulevya. 


Aidha, mkoani Songwe katika eneo la Tunduma, zilikamatwa Kilogramu 8.2 za bangi aina skanka. Dawa hizo 

zilibainika zikiwa zinasafirishwa na mtuhumiwa Lwitiko Kapambila (39) kuelekea Mbeya mjini, akiwa ndani ya 

lori aina ya FAW alilokuwa ameomba lifti kutokea Tunduma.


 

Katika operesheni nyingine zilizofanyika nchini, jumla ya kilogram 707.995 za bangi zilikamatwa. 

Katika kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu na kuzuia uchepushwaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya, 

Mamlaka kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za udhibiti ilifanya ukaguzi katika kampuni zinazojihusisha na 

kemikali bashirifu, maduka ya dawa tiba, kampuni za usafirishaji vifurushi na bandari kavu. 


Kutokana na ukaguzi huo, jumla ya kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu zilizuiliwa kutokana 

na kukiuka taratibu mbalimbali za kisheria. Miongoni mwa Kemikali hizo ni Potassium permanganate,

Hydrochloric acid, Acetone, Sulphuric acid, na Acetic acid glacial. Kemikali hizi endapo zingechepushwa zingeweza kutumika katika mchakato wa kuzalisha dawa za kulevya. 

Aidha, kupitia ukaguzi huo, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya vilikamatwa. 


Dawa hizo ni alprazolam, midazolam, clonazepam, Fentanyl, zolpidem, Tramadol, Codeine na dihydrocodeine. 


"Kitaalam, dawa hizi zinajumuisha makundi ya Benzodiazepini, dawa za kutuliza na kusababisha usingizi, 

pamoja na dawa zenye asili ya afyuni ambazo hutumika kutibu maumivu. Endapo matumizi ya dawa hizi 

hayatadhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha uraibu na utegemezi kwa mtumiaji sawa na dawa za kulevya," amesema.


Amesema kwa ujumla, operesheni za mwezi Machi, 2026 zimeakisi dhamira thabiti ya Serikali katika kukabiliana na tatizo 

la dawa za kulevya nchini. Pamoja na dhamira hiyo, mwenendo wa ukamataji unaonesha uwepo wa mitandao 

mipya ya usafirishaji wa dawa za kulevya hususan mirungi, pamoja na kubadilishwa kwa mbinu za usafirishaji.

No comments:

Post a Comment