BRELA YAPONGEZWA KUSAIDIA WAFANYABIASHARA JIJINI MBEYA - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Saturday, May 30, 2026

BRELA YAPONGEZWA KUSAIDIA WAFANYABIASHARA JIJINI MBEYA


NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuendeleza mkakati kusaidia na kuwawezesha wafanyabiashara vijana, hususan jijini Mbeya kupitia huduma za papo kwa papo.


Mhandisi Mahundi ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la BRELA katika maonesho ya Mbeya City Expo 2026 yanayoendelea mkoani humo ambapo alipata pia fursa ya kuona jinsi Wakala inavyotoa huduma za usajili wa papo kwa papo, hatua inayookoa muda na gharama kwa wafanyabiashara wadogo na wakati.


"Nawapongeza sana BRELA kwa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi wa Mbeya, kutoa huduma za papo kwa papo na kukabidhi vyeti hapa hapa kunawawezesha wafanyabiashara hasa vijana na wanawake kuchangamkia fursa ya kurasimisha biashara zao na kuingia kwenye mfumo rasmi wa kiuchumi," alisema Naibu Waziri Mhandisi Mahundi.


Aidha, akiwa bandani hapo, Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi alipata pia fursa ya kipekee ya kukabidhi cheti cha usajili wa Jina la Biashara kwa mteja aliyekamilisha mchakato wa urasimishaji wa biashara yake papo hapo. 


Nao baadhi ya washiriki na wajasiriamali waliotembelea banda la BRELA walieleza kufurahishwa kwao na huduma ya papo kwa papo inayoendelea kwenye maonyesho hayo, wakisema kuwa imewapunguzia urasimu na kuwapa nafasi ya kulinda nembo na majina ya biashara zao kwa urahisi zaidi.


Maonyesho hayo ya siku kumi yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 30, 2026 ambapo BRELA imekuwa ikitoa huduma za Usajili wa Jina la Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, Leseni za Biashara Kundi A pamoja na elimu ya urasimishaji biashara.

No comments:

Post a Comment