![]() |
NA MWANDISHI WETU
UBALOZI wa Ufaransa kupitia Mradi wa Agro Kilimo unaoratibiwa na Shirika Island of Peace (IDP), umekipatia Kituo cha Maendeleo ya Kilimo na Mazingira Mogabiri (MFEC), shilingi milioni 35 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya kumwagilia mazao yanayolimwa kwa mbinu za kilimo ikolojia.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa MFEC, Peter Mwita wakati akizungumza na waandishi mwishoni mwa wiki ambao walitembelea kituo hicho kilichopo wilayani Tarime mkoani Mara.
Mwita amesema Mradi wa Agro Kilimo umekuwa na faida kwao kwa kuweza kubadilishana uzoefu na wadau wa kilimo ikolojia, kupokea msaada wa miundombinu ambayo inasaidia kuendeleza mashamba darasa ambayo yanasaidia wakulima wilayani Tarime.
"Ubalozi wa Ufaransa kupitia IDP, umetupatia msaada wa shilingi milioni 35 ambazo zimetumika kujenga jengo la kuweka tangi mbili za lita elfu 20 za maji, ambayo yanatumika kumwagilia mashamba ya mfano wakati wa mvua au jua," amesema.
Kaimu Meneja huyo amesema kupitia msaada huo, MFEC inaendelea kuelimisha wakulima umuhimu wa kilimo ikolojia na umwagiliaji.
Mwita amesema marajio yao ni kuona kila mkulima wa Tarime na Tanzania kwa ujumla anajikita katika kilimo ikolojia na umwagiliaji, kwa kuwa kinazalisha chakula safi na rafiki kwa afya ya mlaji.
Amesema wakulima wengi wa Tarime na Mkoa wa Mara watanufaika na mradi huo muhimu, jambo ambalo linawapa nguvu ya kuendelea kutoa elimu.
"MFEC Mogabiri tunazalisha zao la mgomba, sukuma wiki, nyanya, hoho, gabeji, viazi, muhogo na mengine kwa njia ya kiikolojia, hivyo tunawaomba wakulima kujitokeza kwa wingi kuja kujifunza," amesema.
Kaimu Meneja huyo amesema kituo hicho ambacho kimeanza mwaka 1986, pia wanafuga mifugo ambayo inawezesha kuzalisha mbolea ya samadi na mboji.
Mwita amesema kituo kimekuwa kikitoa elimu ya kutengeneza viuatilifu vya asili kwa wakulima wanaofika kujifunza kituoni hapo.
Amesema MFEC imefikia zaidi ya wakulima elfu 35 katika vijiji 33 wilayani humo na kwa saaa wameanza kupokea maombi nje ya mkoa.
Amesema jitihada zao za kuifanya jamii kujikita katika kilimo ikolojia zimekuwa na changamoto kama kupata rasilimali za asili na sera zilizopo kushindwa kuhamasisha jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa IDP, Ayesiga Buberwa amesema Mradi wa Agro Kilimo ni mwendelezo wa kampeni yao ya kuhamasisha mifumo endelevu ya chakula.
Amesema maandalizi ya uzalishaji wa chakula hadi kufika mezani unahitaji ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo MFEC.
Ayesiga amesema Mradi wa Agro Kilimo umejikita kwenye mafunzo na tafiti ambazo zitawezesha wakulima kujikita katika eneo la kilimo ikolojia.
"Mradi huu ulihusisha vituo vya kilimo ikolojia ma tunashukuru Ubalozi wa Ufaransa kufadhili eneo hili muhimu kwa afya ya binadamu," amesema.
Ayesiga amesema mradi huo unawezesha vituo kukaa pamoja, kufundisha wakulima na kuviwezesha vituo vya wakulima.
Mkurugenzi huyo amesema mradi huo umewezesha kupatikana miundombinu ya kukusanya maji ambayo yatatumika kwa muda mrefu kituo hapo.
Ayesiga alitaja vituo vingine ambao vipo kwenye mradi ni SJS Mwanga, RECODA, Shirika la Kilimo Endelevu (SAT), Bihawana Dodoma na PPIZ Zanzibar
Mwakilishi wa Serikali ya Ufaransa, Profesa Jean Luc Paul amesema wamekutoa misaada mbalinbali ikiwemo huo wa Magobiri, ili kuwezesha wakulima kuzalisha mazao ya kiikolojia.
Profesa Jean Luc amesema, Ufaransa imekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta kilimo nchini Tanzania
kuanzia mwaka 1980, hasa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Amesema Ubalozi Ufaransa ulivutiwa na mikakati ya kuendeleza kilimo ikolojia, hivyo ni imani yake mradi huo unaenda kuleta mageuzi chanya kwenye vituo na wakulima kwa ujumla.
" Mradi huu wa Agro Kilimo unaenda kuleta mageuzi kwa wakulima na wasimamizi wa vituo hivi sita," amesema.
Mwakilishi huyo amesema wanashukuru serikali kwa kuwapa ushirikiano chanya jambo ambalo linawapa matumaini kwamba ipo siku wimbo wa kilimo ikolojia utaimbwa na kila mtu.
![]() |









No comments:
Post a Comment