NA MWANDISHI WETU, DODOMA
CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) Leo kimehudhuria uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo huku kikiomba Bunge kusaidia mazingira bora ya kazi kwa wanahabari.
Jowuta imeshiriki kikao hicho cha Bunge kwa mwaliko wa Waziri wa wizara hiyo, Paul Makonda ambaye amewasilisha bajeti hiyo, ambapo amesisitiza suala la uchumi bora kwa vyombo vya habari ili kufanyakazi vizuri.
Amesema wanahabari au chombo cha habari kisipokuwa na uchumi imara ni vigumu kufanya kazi bora kwa kuzingatia maadili.
Hata hivyo amesema Wizara hiyo kupitia bodi ya Ithibati inaendelea kusajiri wanahabari wenye sifa na hadi sasa zaidi ya wanahabari 3000 wamesajiliwa.
Makonda pia aliwafuta machozi baadhi ya wanahabari wakongwe ambao walikuwa wanakosa sifa za kupata Ithibati kwa kueleza utaratibu unawekwa kuwatambua na kuwapatia Ithibati hasa kulingana na uzoefu wao,weledi na kazi walizofanya.
Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusomwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma aliomba Bunge kuzungumzia suala la mazingira bora ya kazi kwa wanahabari.
Juma amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari hawana ajira wala mikataba jambo ambalo linafanya kazi kuwa ngumu.
Amesema licha ya Serikali kutoa agizo la kupandishwa kima cha chini kwa wafanyakazi sekta binafsi lakini bado vyombo vingi vya habari havijapandisha mishahara.
"Tuna imani kubwa na Bunge na Wizara hii kuwa watakuja na suluhu ya kutatua kero za wanahabari na hivyo kufanyakazi katika mazingira bora,"amesema





No comments:
Post a Comment