NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimeingia makubaliana ya kuwapa ujuzi waraibu waliopona matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kujitegemea na kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo ya ushirikiano leo Juni 4,2026 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini, ikiwemo kuzuia biashara haramu ya dawa hizo, kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuimarisha huduma za tiba na urejeshaji wa waraibu katika jamii.
“Ushirikiano na VETA umetokana na kutambua umuhimu wa kuwawezesha waraibu waliopona kupata ujuzi wa kujiajiri na kushiriki shughuli za uzalishaji. Pia ushirikiano huu ni mfano mzuri wa namna taasisi za serikali zinavyoweza kushirikiana katika kutatua changamoto za kijamii kwa manufaa ya taifa,”alisema.
Alifafanua waraibu wengi wanaopata nafuu hujikuta wakirejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya endapo hawapati shughuli za kufanya au mbadala wa kuwawezesha kujipatia kipato. Hivyo, mafunzo ya ufundi stadi yatawasaidia kujenga maisha mapya na kuondokana na mazingira yanayoweza kuwarudisha kwenye uraibu.
Aidha baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wahitimu watawezeshwa kwa vifaa vidogo vya kuanzia kazi kulingana na ujuzi walioupata ili waweze kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato. Pia wataunganishwa na taasisi za fedha zinazotoa mikopo midogo midogo (microfinance) ili kupata mitaji ya kuanzisha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Kamishina Lyimo alisema ushirikiano huo unaendana na mradi wa serikali wa ujenzi wa kituo kikubwa cha urejeshaji na mafunzo kwa waraibu katika Jiji la Dodoma. Kituo hicho kitatoa mafunzo mbalimbali kwa mfumo wa VETA kwa waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa wana uwezo wa kuendelea na masomo ya ufundi stadi.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, waraibu wanaopata matibabu katika kliniki, nyumba za uangalizi maalumu (Sober Houses), hospitali za rufaa na za kanda watapimwa maendeleo yao, na watakapobainika kuwa wamepona kwa kiwango kinachowaruhusu kujifunza, wataelekezwa katika kituo hicho cha Dodoma au kwenye vituo vingine vya VETA vilivyopo nchini.
“Ili kurahisisha mchakato huo, DCEA imeanzisha kitengo maalumu cha Social Welfare Recovery Response, ambacho jukumu lake ni kufuatilia ustawi wa waraibu waliopona, kuwaunganisha na jamii, kuwasaidia kupata mikopo na fursa za ujasiriamali pamoja na kusimamia matumizi ya mitaji wanayopata ili kuhakikisha inaleta tija na kurejeshwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.”
Mamlaka hiyo imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha DCEA na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali za serikali. Ilisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha waraibu waliopona hawarejei tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya, huku wakipata nafasi ya kurejesha heshima yao katika jamii kupitia elimu, ujuzi na ajira.
DCEA pia imebainisha mahitaji ya huduma za matibabu na urejeshaji kwa waraibu yanaendelea kuongezeka nchini, hivyo ushirikiano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuwasaidia wengi zaidi kujenga maisha mapya na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande Mkurugenzi Mkuu VETA CPA.Athony Kasore alisema ushirikiano huo unalenga kuwapa nafasi waraibu waliopata nafuu na kuthibitishwa kuwa tayari kwa mafunzo, ili wapate ujuzi utakaowawezesha kujitegemea kiuchumi. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, wahitimu watakuwa na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa au hata kuanzisha vikundi vya uzalishaji vitakavyotoa ajira kwa wengine.
Aidha, alisema kuwa makubaliano hayo yanakuja kuimarisha juhudi zilizokuwa zikifanyika awali za kuwapatia mafunzo baadhi ya waraibu waliorejeshwa kutoka DCEA. Kupitia mfumo huo rasmi, waraibu wote watakaopokelewa watapatiwa mafunzo, kutambuliwa kwa ujuzi wao na kupewa vyeti vitakavyowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa vyeti vitakavyotolewa vitawasaidia wahitimu kupata fursa mbalimbali za mikopo kutoka serikalini na taasisi za kifedha, hatua itakayowawezesha kuanzisha miradi na biashara za kujiongezea kipato. VETA imeeleza kuwa uwekezaji katika ujuzi ni sehemu muhimu ya kuwawezesha vijana kujenga maisha bora na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma ili kukabiliana na changamoto za kijamii. Pia imewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwahamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi kama njia ya kujenga mustakabali wenye tija kwao na taifa.
.jpg)






No comments:
Post a Comment