MPANGO WA UUNGANISHAJI UMEME KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA WANANCHI – NDEJEMBI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, October 2, 2026

MPANGO WA UUNGANISHAJI UMEME KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA WANANCHI – NDEJEMBI


NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Deogratius Ndejembi, amesema Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, unalenga kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kupata huduma ya umeme kwa urahisi na kwa wakati, ili kuongeza fursa za maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.


Akizungumza leo, Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, Makamu huyo wa Rais amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kutekeleza Mpango wa Misheni 300, unaolenga kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2030 wananchi milioni 300 barani Afrika wanafikiwa na nishati ya umeme.


Amesema kupitia ushirikiano huo, wananchi wanaostahili watanufaika na utaratibu wa kugharamiwa gharama za uunganishaji wa umeme, hatua ambayo itaongeza kasi ya kuzifikia kaya takribani milioni 1.7 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact).


“Ninaipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa hatua hii muhimu ya kuanzisha ushirikiano unaolenga kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya umeme. Ushirikiano huu ni mfano bora wa namna taasisi za umma na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali ili kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja,” amesema Mhe. Ndejembi.


Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amepongeza hatua hiyo na kusema kupitia ushirikiano huo kati ya Serikali na sekta binafsi, wananchi wataendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuwafikishia huduma muhimu ya umeme.


No comments:

Post a Comment