Yanga bado ni kaka kwa Toto - MAGENDELA BLOG

Recent-Post

ads header

Thursday, October 20, 2011

Yanga bado ni kaka kwa Toto

- Yaifyatua 4-2, Tegete amfumbia macho baba'ke
- Azam FC, Polisi Dom kushughulikiana leo
Na Asha Kigundula
MABINGWA wa soka nchini, Yanga nao hawako nyuma kuifukuza Simba kileleni baada ya jana kuifumua Toto Africans ya Mwanza kwa mabao 4-2.
Mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ulikuwa wa upande mmoja tangu kuanza kwa mchezo huo, huku Toto wakionekana kuanza bila kuelewana vizuri katika kila eneo.
Hali hiyo ilianza kuwapa matatizo dakika ya nane ya mchezo, wakati kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima 'Iniesta' alipotumia vizuri makosa ya walinzi wa Toto na kuiweka timu yake mbele kwa bao la kuongoza.
Ni kama walionekana kuchanganyikiwa zaidi, kwani dakika nne baadaye, pasi safi kutoka wingi ya kulia iliyopigwa na Shamte Ally ilisukumwa vizuri na Kenneth Asamoah aliyekosa ulinzi wa kutosha katikati ya mabeki wa Toto.
Kadiri walivyokuwa wakicheza kwa kasi ndivyo walivyowachosha walinzi wa Toto ambao walionekana kama kutojua cha kufanya na kumuacha Jerry Tegete kuwafunga kirahisi bao la tatu kwa kichwa akimalizia kazi ya winga, Idrisa Rashid.
Kutokana na gharika hiyo, Kocha wa Toto, John Tegete alilazimika kufanya mabadiliko ya haraka kuinusuru timu yake, na kuamua kuwatoa kipa Maganfa Seif na kiungo Thony Ndollo na kuwaingiza mlinda mlango, Mustapha Mbarouck na Castory Mumbala, ambaye alionekana angalau kuituliza timu hiyo.
Mabao hayo yaliiongoza Yanga kumalizia dakika 45 za kwanza wakiwa mbele kwa 3-0. Pamoja na uongozi huo, mabingwa hao waliamua kumtoa Idrisa na nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Gumbo.
Yanga iliongeza kasi ya ushambuliaji pamoja na kupata mabao matatu katika kipindi cha kwanza, lakini Toto walikuwa makini katika kipindi cha pili baada ya kuelekezwa mambo muhimu ya kuwakabili mabingwa hao.
Khamis Kiiza aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Tegete angeweza kuiongezea Yanga bao la nne, lakini shuti lake fyongo lilikwenda nje dakika ya 72.
Dakika ya 81, Toto walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Mohamed Soud, baada ya kupokea pasi safi toka kwa Mumbara aliyeonekana kuibadilisha kabisa timu hiyo tangu alipoingia.
Gumbo na Shamte walicheza vizuri na kufanikiwa kuichanganya safu ya ulinzi ya Toto ambao walishindwa kumzuia Asamoah aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, na alifanya hivyo mara baada ya kupokea pasi ya mwisho na kuiandikia Yanga bao la nne  katika dakika za lala salama.
Kwa mshangao mkubwa, nahodha wa zamani wa Yanga, Fred Mbuna jana alipata nafasi ya kucheza tangu kuanza kwa msimu huu akichukua nafasi ya Ibrahim Job, dakika saba kabla ya mchezo kumalizika.
Yanga wakiamini kuwa mchezo huo utamalizika kwa ushindi wa 4-1, Soud alifunga tena bao la pili kwa shuti kali kutokana na safu ya ulinzi ya Wanajangwani hao kushindwa kuamini kuwa mchezaji huyo angeweza kufunga katika eneo alilokuwa, ikiwa imebaki dakika moja mchezo kumalizika.
Mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kujiongezea pointi tatu kwa ushindi wa mabao 4-2, huku ikimkosa kocha wake mkuu, Sam Timbe ambaye inadaiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa maralia.
Kwa matokeo hayo, Yanga imejisukuma katika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 19, ikiwa nyuma ya JKT Oljoro iliyoko katika nafasi ya pili kwenye msimamo kwa pointi 20, wakati Simba ikiwa kileleni kwa pointi 24.
Michezo hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam uliopo Chamazi, Dar es Salaam, ambapo wenyewe Azam FC watakuwa wakiikaribisha Polisi ya Dodoma.

Mchezaji Peter Mutabuzi (kushoto) wa timu ya Toto Africa SC, akimtoka Hamisi Kiiza wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Taifa,  jijini Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda mabao 4-2.
 (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)

No comments:

Post a Comment