Abdulkiba:Zao la waimbaji anayemzimia Dully Sykes - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, December 22, 2011

Abdulkiba:Zao la waimbaji anayemzimia Dully Sykes

Na Hamisi Magendela


NI kawaida kutokea katika tasnia mbalimbali ikiwemo ya sanaa ya muziki kukuta ndugu wawili wakiwa nyota katika kutunga mashairi na kuimba.
Ipo mifano mingi ya wanamuziki waliokuwa wakifanya vizuri na kuipatia sifa kemkem taifa la Tanzania na nje ya mipaka yake.
Hali hiyo haikuanza kipindi hiki, bali hata zamani, waliokuwepo waliweza kushuhidia wanamuziki ndugu wa bendi wakifanya vyema katika muziki wa wakati huo japo ni ngumu kutokea.
kwa sasa, upepo umebadilika na kushuhudia muziki wa kizazi kipya nao ukijumuisha wanandugu kufanya kazi ya aina moja na wakionesha kufanya vizuri na kuwa mfano wa kuigwa kwa watu wengine.
Namzungumzia Abdukareem Saleh 'AbdulKiba', mdogo wanyota wa kibao cha Cindelella 'Alli Kiba', kuwa ni miongoni mwa anayefuata nyayo za kaka yake na kuonesha umahiri mkubwa wa utunzi na kuimba.
"Nitajisikia faraja kama nitaweza kuitangaza vyema nchi yangu ndani na nje ya mipaka yake kwa kutumia muziki, naamini nitafanikiwa kwa maana penye nia pana njia," anasema Kiba.
Msanii huyo anasema alianza harakati za kujihusisha na muziki wa kizazi kipya wakati akiwa shule ya msingi, na ushiriki katika matamasha yaliyokuwa yakifanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumpa mwelekeo mzuri wa kuingia katika tasnia hiyo.
Aliweka wazi kuwa wakati akiwa anapanda jukwaani, watu wengi walifurahia jinsi anavyoweza kumiliki jukwaa na kupangilia sauti yake vizuri na kusababisha wanafunzi waliokusanyika kushuhudia sanaa mbalimbali zilizokuwa zikioneshwa wakilipuka kwa shangwe na vigeregere, kitu kilichompa hamasa kuwa anaweza.
Baada ya kugundua kuwa ana kipaji cha kuimba na kusababisha kuvuta mashabiki wengi na kuona kaka yake akiwa katika safari hiyo ya muziki na kufanya vyema, akaona ajiingize rasmi katika tasnia hiyo.
Na ujio wake wa kazi yake ya kwanza ikawa ni 'Najua Ni Kipi' na kurekodiwa katika studio ya Mazoo, ambao umo katika albamu ya kwanza ya Alli Kiba.
Anasema katika watu waliompa moyo na kumsaidia katika kazi zake nyingi ni wengi kwa uchache ni pamoja na msanii Dully Sykes, Alli Kiba, wasanii wengine pamoja na mashabiki kwa kumshauri kufanikisha muziki wake kufika mbali zaidi na uweze kutambulika kimataifa.
Msanii huyo kwa sasa anatamba na vibao vyake kadhaa ikiwa ni safari ya kuelekea kufyatua albamu yake ya kwanza ikitarajiwa kuwa na nyimbo lukuki zenye mafundisho kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Moja ya kibao kinachofanya vizuri ni pamoja na 'Siyo Demu', kilichotengenezwa katika studio ya Mazoo na kuwashirikisha vyema Neiba pamoja na Ney 'Wa Mitego', na kufanya vyema katika vituo mbalimbali vya redio.
Hakika kibao hicho kimeweza kumtambulisha vyema katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya na kumuweka katika taswira ya wasanii wachache wanaofanya vizuri na kuonesha umahiri wao wa kufikiri na kutunga mashahiri yanayosisimua jamii.
Abdulkiba anasema katika tasnia muziki, kitu kikubwa asichokipenda ni pale inapotokea baadhi ya wasanii wakawa na mikwaruzano, ambayo husababisha kupoteza maisha na kuonekana fani hiyo ni ya kihuni.
"Inasikitisha kuona wanagombana na kurushiana maneno yasiyo ya msingi wakati kwangu naona muziki ni sehemu ya furaha na kuendeleza amani sehemu yoyote ile duniani, hivyo ni vyema wasanii wezangu tukawa kitu kimoja ili kuweza kuendeleza muziki wetu mbele," anasema msanii huyo. 
Anasisitiza kuwa ni vyema wasanii wakaishi kwa kuvumiliana na upendo, na siku zote binadamu ana mapungufu na ndiyo ubinadamu ulivyo kwa kwa maana katika dunia hakuna aliyekamilika.
Anasema tangu aanze kuingia katika muziki, amefanikiwa kujiendeleza kimaisha na kufahamika na jamii kubwa zaidi kuliko alikuwa awali kabla ya kuwa msanii.
Aliweka wazi kuwa kutokana na wasanii kuwa kioo kwa jamii na kupendwa na watu wa aina mbalimbali, Abdulkiba ametoa wito kwa wasanii wenzike kujiepusha na anasa kwani siku zote mwisho wake ni mbaya.
Dully Sykes ndiye msanii anayemvutia zaidi katika muziki wa Bongo Fleva kutokana na umahiri wake katika ubunifu wa muziki wake na kumfanya kila anapotoka na wimbo mpya kuonekana yuko juu kuliko wasanii alioanza nao.
Abdulkiba, kwa sasa yupo mbioni kuachia kibao kingine kinachokwenda kwa jina la Kizunguzungu, ukiwa umetayarishwa katika studio ya Mazoo.

Abdull Kiba akiwa katika pozi

No comments:

Post a Comment