Kili Stars yachomoa Mapinduzi Cup - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, December 23, 2011

Kili Stars yachomoa Mapinduzi Cup

- TFF yadai haina wachezaji wa kutosha
- Kuandaa timu kuivaa Misri Februari
Na Asha Kigundula
MCHEZO uliopangwa kuwa wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kati ya timu Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' na ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' uliokuwa ufanyike Disemba 31 mwaka huu umevunjika.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah, alisema wameshindwa kuaandaa timu hiyo baada ya timu zenye wachezaji wengi katika timu hiyo nazo kushiriki michuano hiyo.
Osiah alisema licha ya wachezaji wa timu za Azam Simba na Yanga kuwepo kwenye timu hiyo, bado wana wachezaji wachache wengi wa kuweza kuunda kikosi kamili cha Kilimanjaro.
Alisema licha ya kutoweza kuandaa timu ya kushiriki katika mchezo huo, hata makocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' na Charles Mkwasa nao wana majukumu mengine.
Alisema Mkwasa kwa sasa yupo na timu ya Taifa ya soka ya Wanawake 'Twiga Stars' katika maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Namibia, wakati Kihwelo akiwa nje ya nchi.
Alisema tayari wameshawasiliana na viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuhusiana na kutoshiriki kwao katika mchezo huo wa ufunguzi.
Osiah aliongeza kuwa wameshatuma barua pepe (email) kwa ajili ya kuwafahamisha kutoshiriki mchezo huo, ambapo sasa wanajipanga kucheza mchezo wa kirafiki wa kusaidia wahanga wa ajali ya meli ya MV Spice Islander.
Wakati huo huo, Chama cha Soka cha Misri (EFF) kimetuma maombi ya  mchezo mmoja wa kirafiki na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ufanyike nchini kwao kati ya Februali 23 na 24.
Osiah alisema Misri imeomba mchezo huo wa kirafiki ambapo watalipa gharama zote za timu hiyo ikiwa nchini humo pamoja na usafiri wa kwenda na kurudi nchini humo.
Alisema tayari wamekubali kucheza mechi hiyo ambayo itasaidia kuendelea kuifua timu yao kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil 2014.