Wabunge Kanda ya Kati kushuhudia Miss Utalii - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Thursday, December 22, 2011

Wabunge Kanda ya Kati kushuhudia Miss Utalii

Na Asha Kigundula
WABUNGE wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa majimbo ya mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora ni miongoni mwa waalikwa maalum watakaoshuhudia mashindano ya Miss Utalii Vyuo Vikuu 2011/12 - Kanda ya Kati.

Mashindano hayo makubwa yanatarajiwa kufanyika Desemba 30 kwenye Ukumbi wa Club La Azziz, uliopo mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Emanuel Msangi, Katibu Mtendaji wa Miss Tourism Tanzania Organisation- Kanda ya Kati, ilisema lengo la kuwaalika wabunge hao ni kutoa hamasa zaidi kwa viongozi, wananchi na Taifa kwa ujumla juu ya umuhimu wa Utalii katika uchumi wa taifa na Jamii.
Pia, uwepo wao utasaidia kuhamasisha zaidi jamii juu ya utalii wa ndani na utalii wa kitamaduni.
"Ni matarajio yetu kuwa baada ya mashindano haya, wabunge, wataongeza kasi ya kuhamasisha utalii wa ndani na wa kitamaduni katika majimbo yao, kwani utalii ni moja ya sekta madhubuti katika kupambana na umasikini na tatizo la ajira katika jamii," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wakuu wa wilaya na mikoa yote iliyopo Kanda ya Kati pia wamealikwa kuhudhuria mashindano hayo, ambapo yanashirikisha warembo kutoka katika vyuo vikuu vilivyopo katika mikoa ya Singida, Dodoma, Tabora na Morogoro.
Tayari kambi ya mazoezi imeanza katika Hotelii ya kisasa ya NAM mjini Dodoma chini ya mkufunzi wao, Mariam Hamisi (Miss Utalii Dodoma 2010/11 na mshindi wa Taifa wa tuzo ya ya Jinsia Miss Utalii Tanzania 2010/11- Gender).
Viingilio katika shindano hilo ambalo litakuwa na ulinzi wa kutosha kwa watu na magari siku hiyo vitakuwa ni sh 200,000 kwa meza ya watu 10, sh 100,000 kwa meza ya watu 4 na sh 60,000 kwa meza ya watu 2. Tiketi zake zitaambatana na chakula cha jioni isipokuwa kwa watakaokata tiketi za sh 10,000.

No comments:

Post a Comment