Lundenga awafunda miss Kurasini
Na Dotto Mwaibale
WAREMBO wanao jiandaa na shindano la Redd's Miss Kurasini 2012 wametakiwa kulinda heshima zao ili jamii isiwachukulie ni wahuni.
Rai hiyo ilitolewa juzi Ukumbi wa Eguator Grill Mtoni kwa Azizi Ali Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency, Hashim Lundenga, ambayo ni waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania alipokuwa akiwafunda warembo hao.
"Urembo si uhuni kama baadhi ya watu katika jamii wanavyodhani na mawazo hayo yanatokea kufuatia tabia ya warembo husika kufanya mambo ya ajabu mbele ya jamii" alisema Lundenga.
Alisema wapo baadhi ya warembo wanajiingiza katika fani hiyo kwa ajili ya kutimiza malengo yao yanayokwenda kinyume na kanuni za kamati za miss Tanzania.
"Kuna baadhi ya warembo wameingia katika fani hii kwa ajili ya kufanya mambo ya ajabu ambayo hayaleti sifa nzuri miongoni mwa jamii inayotuzunguka hatutakubali kuwa na warembo wa namna hiyo" alisema Lundenga.
Lundenga alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya waratibu wanaowataka kimapenzi warembo hao kwa kuwashawishi kuwa watashinda kuwa wasisite kutoa taarifa ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.
"Kuna baadhi ya waratibu wamekuwa na tabia ya kuwatakeni kimapenzi wakidai watawasaidieni kushinda watajeni kwani ni kosa kufanya hivyo" aliongeza Lundenga.
Aliwataka warembo hao kuvaa nguo zenye heshima badala ya kuvaa zile zinaonesha maungo yao ya ndani na kuwataka kujiamini kwa kila jambo na kuongea kwa ufasaha kwa lugha ya kiingereza na kiswahili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda.
Shindano hilo linatatarajiwa kufanyika kesho katika ukumbi wa Equator Grill, Mtoni kwa Azizi Alli.
Tuesday, May 22, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment