Masikini Kajala!
Na Grace Gurisha
MSANII wa filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe Faraja Mchambo, wataendelea kusota rumande hadi hakimu anayesikiliza kesi yao amalize likizo ya uzazi.
Kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri, ambapo kuna mashahidi watatu.
Hakimu Mkazi, Frank Moshi, alisema ombi la upande wa utetezi la kutaka kesi hiyo apewe hakimu mwingine limekataliwa na kudai kuwa litaendelea kusikilizwa na hakimu Sundi Fimbo, ambaye ndiye aliyekuwa anasikiliza shauri hilo.
Alisema amepokea jalada hilo kwa ufafanuzi kuwa jalada haliwezi kupewa hakimu mwingine, kwa sababu anaweza akapewa hata hakimu mwingine naye akaondoka.
Pia, alidai kuwa waliwasiliana na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, IIvin Mgeta, kuhusu uamuzi wa suala hilo, lakini uamuzi ni kwamba jalada haliwezi kwenda kwa hakimu mwingine kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.
"Kesi hiyo itaendelea kutajwa hadi hakimu anayesikiliza kesi hiyo atakaporudi likizo, kwa hiyo imeahirishwa hadi Juni 5 mwaka huu, kwa kutajwa," alisema Moshi.
Upande wa Jamhuri, alikuwepo wakili Secilia Mkonongo na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Kwa mujibu wa mashtaka yao, wawili hao wanadaiwa katika shtaka la kwanza Aprili 2010, jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuhamisha umiliki wa nyumba.
Shtaka la pili walidaiwa wote kwa pamoja walihamisha umiliki wa nyumba hiyo iliyoko Kunduchi jijini Dar es Salaam wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Katika shtaka la mwisho, wanadaiwa kufanya uhamisho wa umiliki wa nyumba hiyo Julai 14 2010 jijini Dar es Salaa, huku wakijua kuwa ilipatikana kwa fedha chafu za rushwa.
No comments:
Post a Comment