Samata, Ulimwengu wainogesha Stars
Na Asha Kigundula
WACHEZAJI wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu, wamejiunga na kambi ya timu ya Taifa inayojiandaa na mechi dhidi ya Ivory Coast, mchezo utakaofanyika Juni 2 mjini Abijan.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema tayari wachezaji hao wamesharipoti na kuingia kambini.
Wambura, alisema Samata na Ulimwengu wanajiunga katika kambi hiyo wakitokea mjini Lubumbashi nchini Congo (DRC) katika timu yao ya TP Mazembe, ambayo wanaichezea.
Alisema kuwa licha ya kuripoti kwa wachezaji hao, pia mshambuliaji wa Simba, Haruna Moshi 'Boban', aliyekuwa mazikoni mjini Kinshasa, amewasili juzi usiku.
Alisema kwa upande wa Boban, amerejea akitokea Kinshasa alikokwenda kwa ajili ya mazishi ya mchezaji mwenzake katika klabu ya Simba, Patrick Mafisango, ambaye alifariki wiki iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea Keko, Dar es Salaam.
Timu hiyo iliyopo chini ya kocha Kim Poulsen, ipo kambini kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ivory Coast.
Kabla ya mchezo huo, Stars itakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Malawi, itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi.
cccc
TFF yawatibua wazee Yanga
- Waitaka kuangalia pande zote
- Watishia kuisajili Yanga ZFA
- Kamati ya Utendaji sasa wabaki 3
Na Julius Kihampa
HALI ndani ya klabu ya Yanga imezidi kuwa ngumu kutokana na Baraza la Wazee kuendelea kushikilia msimamo wao kushinikiza kumuondoa Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga.
Juzi, wakati wazee hao wakikutana na kundi kubwa la wanachama na kupitisha maazimio ya pamoja ya kumuengua Nchunga, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah, aliitaka klabu hiyo kusimamia katiba yao.
Kwa mujibu wa Osiah, Yanga ingekuwa imekiuka baadhi ya vipengele katika katiba yao kama wangeshinikiza kumng'oa madarakani Nchunga, ambaye anashutumiwa kwa makosa kadhaa ya kuigharimu Yanga.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, alisema kauli ya Katibu wa TFF imeegemea zaidi upande mmoja na kuiumiza klabu.
Akilimali, alisema Osiah ameiona Yanga kama isiyofuata katiba yao iliyofanyiwa marekebisho 2010, kitu ambacho kimeonesha kuegemea upande mmoja na kushindwa kujua kama wanaoumia ni wanachama.
"TFF ni kama baba, na wanachama wa Yanga ni kama wake, ambao mume hapa anakuwa uongozi unaoongozwa na Nchunga, na kama mke anapeleka matatizo ya mumewe kwa baba, na anyepelekewa anaonesha kuwa upande wa mume, hii sio sawa.
"Ikumbukwe kwamba Yanga ni ya wanachama. Nchunga hakufanya mikutano ya kujua mapato na matumizi kwa miaka yote miwili aliyokuwa madarakani, bado klabu ina madeni, na ameshindwa kuwazuia wanachama waliokimbilia mahakamani, hii si sawa," alisema Akilimali.
Alisema katika ibara ya 33, ukurasa wa 22 (kifungu F), Mwenyekiti wa Yanga anatakiwa kuongoza na kusimamia kila jambo la maendeleo ya klabu hiyo.
Lakini alidai kuwa, kiongozi huyo na kamati yake ya utendaji imeshindwa kabisa kukidhi majukumu hayo kwa kuiachia klabu madeni makubwa. Na kufungu cha tano cha ibara hiyo, kikisema 'Mwenyekiti anayeshindwa kutimiza majukumu yake, anatakiwa kukaimisha madaraka kwa makamu.
"Lakini kwa bahati mbaya sisi hatuna makamu mwenyerkiti, hivyo tunatakiwa kuangaliwa tena na TFF, ambao kama baba walitakiwa kutusaidia katika hili, na si kusikiliza upande mmoja na kutoa kauli za kutukandamiza," alisema mzee Akilimali.
Akifafanua hatua ambayo wamechukua baada ya kauli ya Osiah, kiongozi huyo alisema wamepeleka kwa maandishi malalamiko yao kwa TFF, kwa Msajili wa Vyama vya Michezo Ilala, Kamati ya Usajili ya Yanga na kwa Tume ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya uchunguzi wa ubadhilifu wa fedha zao.
"Tumeangalia kwa kina na tuna uhakika kuwa kutokana na kodi ndogondogo ambazo klabu inakusanya, inaingiza kiasi cha sh. milioni 52, lakini tunashindwa kujua ni kwanini tunashindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake," aliongeza.
Akizungumzia juu ya kauli ya katibu wa TFF, mzee Akilimali, alisema wameazimia kutoa siku moja kuona kama TFF itakuwa na msaada kwao katika jambo hilo, na vinginevyo wataisajili timu ya Yanga katika Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kucheza ligi ya huko.
Wakati hali ikiwa hivyo, Nchunga amezidi kupata pigo katika safu yake ya kamati ya utendaji, ambapo sasa, katika jopo la wajumbe 13, wamebaki watatu pekee, huku wengine wanne wakitangaza kujiuzulu jana.
Kwa mujibu wa mzee Akilimali, Yanga inadaiwa na wachezaji wake wa zamani sh. milioni 106, ambazo uongozi wa Nchunga umeshindwa kuondoa deni hilo, huku baadhi ya wafanyakazi wengine wa benchi la ufundi wakidai mishahara yao ya miezi kadhaa iliyopita.
Tuesday, May 22, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment