- Afungua kesi kwa kuvamiwa
- Manji arudisha udhamini
Na Asha Kigundula
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga Lloyd Nchunga, jana ametangaza kujiuzulu wadhifawa wake kuingoza klabu hiyo.
Nchunga, ameingia matatizoni na kuifanya klabu ya Yanga kushindwa kuwa tulivu hasa baada ya kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Simba, huku mengi yakiibuka yakiwemo ya kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa wanachama tangu aingie madarakani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Nchunga, alisema ameamua kuachia ngazi ili kuinusuru klabu hiyo ambayo ilitaka kufikia hatua mbaya kwa kudaiwa kutotimiza majukumu yake kama mwenyekiti.
Nchunga alisema kuna baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walionesha wazi kuisaliti klabu hiyo kwa kauli zao, lakini yeye kama mwanachama wa klabu hiyo ameona ni bora akae pembeni huku Kamati ya Utendaji ikimteua mwenyekiti mpya wa kuingoza klabu hiyo.
Alisema anajua taarifa ya kuondoka kwake kuna wanachama na wajumbe wa Yanga itawafedhehesha, hasa ukizingatia uamuzi wa pamoja wa vikao vyao vya kamati ya utendaji vilivyopita waliambizana kuwa hakuna atakayejiuzulu.
Nchunga alisema tangu walipoingia madarakani walishirikiana vizuri na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, ambayo ni Ngao ya Hisani (2010), Ubingwa wa Ligi Kuu (2011-12) na wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup).
"Nichelee kusema tu kuwa tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti, Davis Mosha, na wajumbe Seif Seif, Ally Mayayi na hata alipooondoka mdhamini mteule, Yusuf Manji, ambaye sasa ameonesha nia ya kurudi," alisema Nchunga.
Aliongeza kuwa kamwe hawezi kumlaumu mchezaji mmoja-mmoja, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo wao dhidi ya watani zao, Simba, inaonesha kulikuwa na usaliti mkubwa ambao hawakuweza kuubaini.
Alisema si kweli kwamba wachezaji kudai posho na mishahara iwe chanzo cha vurugu zilizoibuka, wala kuwepo na ukweli kwamba mtendaji wao mmoja alishikiliwa Arusha kwa ajili ya kutoa kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Simba.
"Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula wenyewe kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuondoa uongozi wa kidemokrasia," alisema.
Lloyd Nchunga aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Yanga ambaye ametangaza kujiuzulu Dar es Salaam jana. |
"Lakini unaweza kuona kuwa yule ambaye alikuwa mama halisi wa mtoto aliona uchungu na kuamuru apewe yulea siye wake. Kwa maana hiyo, nimeamua kukaa pembeni kutokana na mapenzi ya dhati kwa klabu hii," aliongeza.
Kiongozi huyo alisema anaamini kuwa kamati ya utendaji pamoja na wale waliochaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 29 (3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini itawaongoza wanachama hadi kufikia mkutano mkuu wa klabu hiyo Julai 15.
Licha ya kutangaza kujiuzulu, Nchunga, ambaye amefaidi madaraka ya klabu hiyo kwa miaka miwili, amesema ataendelea kuwa mwanachama muadilifu wa Yanga.
Na katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema amefungua kesi mahakamani kutokana na kuvamiwa juzi nyumbani kwake na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa Yanga, na uchunguzi wake unaendelea.
ciooo
Makalla aitaka Twiga kushinda ugenini
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imeondoka jana kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia na kukabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
Twiga Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi, itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya kwa fainali za nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC), zitakazofanyika Novemba mwaka huu Guinea ya Ikweta.
Mechi hiyo itafanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Addis Ababa, wakati ile ya marudiano ikiichezwa Juni 16 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imapeta tiketi ya kwenda Guinea ya Ikweta.
Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
![]() |
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars |
Twiga Stars, ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA), ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lina Mhando, itarejea nchini Jumatatu mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
ciooo
Nani kutwaa taji la Redd's Miss Kurasini leo
Na Hamisi Magendela
WANYANGE 16 wanatarajiwa kupanda jukwaani usiku huu kumsaka kinara wa mashindano ya Redd's Miss Kurasini 2012, kinyang'anyiro kinakachofanyika kwenye Ukumbi wa Equator Grill, Temeke, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mratibu wa mshindano hayo, Yason Mashaka, alisema maandalizi yamekamilika na burudani kutopka kwa malkia wa mipasho nchini, Khadija Kopa na bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia watakuwepo kuwasindikiza warembo hao.
"Wadhamini mbalimbali wamejitokeza kudhamini ambao kwa njia moja au nyingine wamefanikisha kukamilika kwa shughuli hii, na kesho (leo) ndiyo tunamtoa mshindi mpya wa Redd's Miss Kurasini," alisema Mashaka.
Taji la Miss Kurasini anayemaliza muda wake linashikiliwa na Mwajabu Juma, ambaye alifanikiwa kukiwakilisha vyema kwa kushiriki katika fainali za Redd's Miss Temeke 2-11, na alikuwa miongoni mwa waliongia nusu fainali na kujinyakulia taji la Top Model.
Mashaka aliwataja washiriki wa mashindano hayo kuwa ni Mariam Sadic (19), Linda Deus (20), Neemadoree Sylvester (29), Lindanacy Joseph (20), Betty Peter (22), Lilian Joseph (20), Christina Moses (20), Fraviana Maeda (22).
Wengine ni Sia Kimambo (19), Angel Gasper (19), Farida Mrope (23), Jennifer Njabili (18), Elizabeth Mkende (19), Edina Magige (22), Irene Sostheness (20) na Johari Juma(20).
Warembo hao wamefundwa vilivyo na wakufunzi wao Mwajabu Juma na Rose Hurber.
No comments:
Post a Comment