Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla akizungumza na wachimbaji wadogo wadogo katika mgodi wa dhabau wa Itumbi kata ya Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya Februari 2 mwaka huu. |
Na Emanuel Madafa, Mbeya
Serikali Mkoani Mbeya imeahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya askari Polisi wanao tuhumiwa kuhusika na ubebaji wa mawe ya dhahabu katika shughuli za uokoaji wa wachimbaji waliofukiwa na kifusi mwezi February mwaka huu Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.
Hatua hiyo inakuja kufuatia baadhi ya wachimbaji madini wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Itumbi Kata ya Matundas Wilayani Chunya kutoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makalla, ambaye alifika katika eneo hilo kujionea hali halisi ya maafa hayo, ambapo inaelezwa kuwa zaidi ya wachimbaji wadogo 25 katika mgodi wa dhahabu wa Itumbi,walifukiwa na kifusi na kusababisha majeruhi na vifo vya watu wanne, mwezi February mwaka huu.
Wachimbaji hao walidai mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa baadhi ya askari polisi ,walishindwa kutekeleza wajibu wao katika kufanya kazi ya uokoaji wa watu na mali zao, badala yake wao walikimbilia kubeba mawe ya dhahabu ambayo yalikuwa tayari yamechimbwa na wachimbaji hao, kisha kuyapakia kwenye gari ya polisi na kuyasafirisha mahala pasipojulikana.
Wachimbaji hao, walimweleza Makalla kuwa askari hao ambao wanadaiwa kuwa si waadilifu, wao waliendelea na shughuli ya ubebaji wa mawe ya dhahabu ambayo yalikuwa yamechimbwa na wachimbaji na yapo nje yakisubili kuchenjuliwa ili kupatikana madini aina ya dhahabu.
Aidha, kutokana na malalamiko hayo, Makalla aliwataka wananchi pamoja na wachimba madini hayo kuwa watulivu na wapole, kwa kuwahakikishia kwamba serikali italishughulikia suala hilo na kuwachukulia hatua baadhi ya askari watakaothibitika kuhusika na tuhuma hizo.
“Serikali haitalinyamazia suala hili, nimeunda kikosi kazi cha watu kadhaa ambao watayafanyia kazi malalamiko haya na kama kutakuwa na ushahidi wa bila kuacha shaka juu ya askari kuhusika na ubebaji wa mawe ya dhahabu, basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa sambamba na kufikishwa mahakamani,”alisema.
Amesema, wakati zoezi hili linafanyika, serikali imeufunga mgodi huu wa Itumbi, na kuwataka wachimbaji kutofanya shughuli yoyote kwani mbali na maafa yaliyotekea pia mgodi huo umeghubikwa na changamoto nyingi, ukiwemo mgogoro baina ya wananchi na mfanyabiashara Vicent Minja juu ya nani mmiliki halali wa eneo la mlima huo unaosemekana kuwa na madini aina ya dhahabu.
Mwisho.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wadogo katika mgodi wa Itumbi kata ya Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya akitoa malalamiko yake mbeya ya Mkoa wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla (hayupo Pichani). |
Mkutano ukiendelea. |
No comments:
Post a Comment