Na: Mwandishi Wetu - Dodoma
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutatua
changamoto za wafanyakazi ili kuboresha maslahi yao.
Waziri
Ndalichako ametoa kauli hiyo leo Septemba 15, 2022 wakati akifungua
semina ya siku moja kwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusu
uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni katika ukumbi wa PSSSF,
jijini Dodoma.
Amesema kuwa, Rais Samia anawajali na kuwathamini
wafanyakazi kutokana na mchango wao mkubwa wanaotoa katika ujenzi wa
uchumi wa nchi na ndio maana anataka kila mtumishi aweze kushiriki
kikamilifu katika kukuza maendeleo ya nchi.
“Ninyi nyote ni
mashahidi katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu
Hassan watumishi wameweza kupandishwa madaraja vilevile ajira
zimetangazwa kwa wingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu”
“Nimshukuru
Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uamuzi wa kulipa
shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kulipa deni lililodumu kwa muda
mrefu la shilingi trilioni 4.6 la michango kabla ya 1999 kama malipo ya
deni la Serikali kwa lengo la kukomboa mifuko,”
Aidha, Waziri
Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwasisitizia viongozi hao wa Vyama vya
Wafanyakazi juu ya umuhimu wa kuendelea kutoa na kueneza elimu hiyo ya
Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyoanza kutumika Julai 1, 2022 kwa
wanachama nchi nzima.
Sambamba na hayo, Mhe. Ndalichako amewataka
viongozi hao kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuleta tija na
ufanisi katika kukuza sekta ya kazi na ushughulikiaji wa masuala ya
wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama
vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema kuwa semina
hiyo itasaidia kuwajengea uelewa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi juu
ya Kanuni hiyo mpya ya mafao ya pensheni, ili waweze kukuza uelewa wa
wanachama kuhusu kanuni hiyo kwa wanachama wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) wakati wa ufunguzi wa semina ya uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Septemba 15, 2022, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment