NA MWANDISHI WETU
UONGOZI wa Chuo cha Ufundi Stadi Furahika kinachopatikana Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kimetoa salamu za pole kwa familia ya Rais wa Serikali Mapinduzi Zanzibar kutokana na kifo cha Abbas Mwinyi, ambaye ni kaka wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Alli Mwinyi .
Mkuu wa Chuo hicho Dkt. David Msuya, ametoa pole hiyo leo, Septemba 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na akafafanua kwamba uongozi wa chuo hicho upo bega kwa bega na familia ya Dkt Mwinyi katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.
Abbas, ambaye pia ni mtoto wa marehemu Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi, alikuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Fuoni, Zanzibar alifariki dunia jana katika Hospitali ya Lumumba mjini Unguja na amezikwa leo katika eneo la Bweleo na kuhudhuriwa viongozi mbalimbali visiwani humo.
“Sisi Chuo cha Furahika kwa masikitiko makubwa tunatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Alli Mwinyi na familia kwa ujumla kwa kuondokea na kaka yao, hivyo tunamuomba Mungu ampe nguvu katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho ya marehemu Abbas, mahala pema peponi ,” amesema.
Marehemu Abbas kabla ya umati, alikuwa mgombea aliyeteuliwa na CCM kuwania ubunge katika Jimbo la Fuoni, ingawa awali alikuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2015 na katika uchaguzi wa mwaka huu alikuwa anatetea kiti hicho.
No comments:
Post a Comment