MGOMBEA UDIWANI KATA YA KURASINI AAHIDI NEEMA KWA WANANCHI - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Tuesday, September 30, 2025

MGOMBEA UDIWANI KATA YA KURASINI AAHIDI NEEMA KWA WANANCHI


NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Kurasini Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Selestine Nyakunga amesema moja ya mikakati yake pindi atakapochaguliwa kuwa diwani katika uchaguzi mkuu ujao, wananchi wake wataendelea kunufaika na ajira kupitia uwekezaji wa viwanda ambavyo vipo katika eneo hilo.

Nyakunga amefafanua kwamba anaamini moja ya changamoto ambayo ipo kwa wakazi wa eneo hilo hususan kwa vijana ni ukosefu wa ajira, hivyo atakapofanikiwa kuwa diwani wa kata hiyo atahakikisha anazungumza na wamiliki wa viwanda kutoa kipaumbele kwa wananchi wa eneo hilo pindi zinapotokea nafasi za ajira.

“Kwanza nimshukuru Dkt Samia Suluhu Hassan kwani tangu aingie madarakani kwa nafasi ya urais, Kurasini kumekuwa na ongezeko la uwekezaji wa viwanda jambo linalochochea maendelea kwa kasi kubwa, kutokana na uwekezaji huo pindi nitakapofanikiwa kuwa Diwani wa kata hii.

 “Nitaweka mkakati wa ajira zipitie kwenye ofisi ya diwani ili itoe fursa kwa vijana wetu  kuchukua nafasi hizo kutoka kwenye viwanda vilivyopo katika kata hii na zile ajira ambazo vijana wetu hawatakuwa na sifa zitaende nje ya kata yetu,” amesema.

Pia amefunguka kuwa katika kipindi chake cha uongozi wake atahakikisha anahamasisha kundi kubwa la vijana wa kata hiyo, wanakwenda kusoma katika vyuo vya ufundi ili wapate ujuzi wa kuendesha mitambo katika viwanda vilipo katika eneo hilo pindi fursa za ajira zinapotokea.

Kada huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo anakishukuru chama chake kwa kumteua kuwania nafasi ya udiwani baada ya michakato kadhaa ya uteuzi kupita na akaweka wazi kwamba atahakikisha anaendeleza miradi yote iliyoachwa viporo na mtangulizi wake katika nafasi hiyo.

Aidha anaweka wazi kuwa anaamini mtangulizi wake amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha miradi ya maendeleo  inafanya vizuri chini ya Ilani ya CCM, hivyo ameahidi kuendeleza alipoishia na kutekeleza kikamilifu mingine ili kuleta tija kwa wananchi wa kurasini.

“Nawaomba wananchi wa Kurasini wahakikishe Oktoba 29 mwaka huu wanapiga kura za kutosha kwa mgombea wetu wa urais Dkt Samia, mbunge wetu na kwangu kwa nafasi ya udiwani ili tuweze kusukuma gurudumu la maendeleo kwa pamoja”, amesema.

 

 

No comments:

Post a Comment