WAZIRI
wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameruhusu Magari kuanza
kutumia daraja jipya la wami kufuatia Ujenzi wake kukamilika.
Profesa
Mbarawa amewataka viongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani, Kuhakikisha
daraja hilo linalindwa ili kudumu kwa zaidi ya miaka 120 iliyokusudiwa
kutumika.
"daraja
limekamilika kwa asilimia 96 hivyo madereva na watumiaji wa daraja
hili, tumieni kwa uangalifu na kulitunza kwa kuwa kazi ndogo ndogo za
ukamilishaji zikiendelea." amesema Prof.Mbarawa.
Aidha,
Prof. Mbarawa amewataka viongozi kutoa ushirikiano kwa Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS) na wakandarasi wanaojenga barabara ya magari
yaendayo haraka ya Kibaha-Chalinze-Morogoro Express Way (km 215)Ili
kuwezesha Ujenzi kuanza kwa wakati.
"Serikali
inaendelea kuufungua mkoa wa Pwani kwa kuendeleza Ujenzi wa barabara
kutoka Pangani-Horohoro-Lungalunga- hadi Mombasa nchini Kenya ambayo
itaboresha uchumi wa viwanda na kukuza utalii katika eneo hilo la
kimkakati," ameongezea Profesa Mbarawa.
Kwa
Upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS), Eng. Dorothy Mtenga, amesema zaidi ya shilingi bilioni 75
zimetumika katika Ujenzi wa daraja hilo lilokusudiwa kutatua changamoto
za daraja la mwanzo ambalo lilikuwa halikidhi mahitaji ya magari
yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita na lilikuwa na njia
moja.
Naye
Mkuu wa Wiaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Abdalah Issa, ameishukuru
Serikali hususani Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa utekeleza wa miradi
ya miundombinu ya kimkakati katika Mkoa wa Pwani, inayochochea maendeleo
ya Viwanda, Utalii na Biashara.
Aidha, amemhakikishia Waziri Mbarawa, kuwa madaraja na barabara zinazojengwa katika mkoa wa Pwani, zitatunzwa vizuri.
Kwa
upande wake Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameishukuru
Serikali kwa kuendeleza miradi ya miundombinu katika mkoa wa Pwani ili
kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Daraja
jipya la Wami, lenye urefu wa mita 513.5, upana mita 11.85 na barabara
unganishi km 3.8 linaunganisha mkoa wa Pwani na Tanga, litachochea
ustawi wa jamii kiuchumi na kuleta maendeleo kwa mikoa ya kaskazini mwa
Tanzania.
(Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)
No comments:
Post a Comment