TANI 850,000 ZA MBOLEA ZINAHITAJIKA NCHINI MSIMU UJAO - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Monday, July 17, 2023

TANI 850,000 ZA MBOLEA ZINAHITAJIKA NCHINI MSIMU UJAO


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dk. Stephan Ngailo wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dkt. Stephani Ngailo  akiwa kwenye moja ya maghala ya mbolea katika mkoa wa Njombe  kwa lengo la kujionea upatikanaji wa mbolea nchini itakayotumika katika msimu wa  kilimo wa 2023/2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti  wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo akizungumza na vyombo vya habari  leo jijini Dodoma wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo kwa mwaka 2022/2023 na vipaumbele kwa mwaka 2023/2024.

** *******

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo amesema mahitaji ya mbolea kwa mwaka 2023/24 ni tani 850,000 na mpaka sasa asilimia 45 ya mbolea inayohitajika tayari iko nchini.

Dk Ngailo ameyasema hayo leo tarehe 17.07.2023 jijini Dodoma  wakati wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TFRA na mwelekeo kwa mwaka 2023/24.



Alisema Mamlaka itaendelea kutekeleza vipaumbele vya kuratibu upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini tani 850,000 na kuratibu na kusimamia utekelezaji wa utoaji wa mbole ya ruzuku ambao umetengewa Sh bilioni 150.



Dk Ngailo alisema pia Mamlaka itaendelea kudhibiti ubora wa mbolea na kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini.



“Pia kushirikiana na wadau kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na uimarishaji wa maabara ya uchambuzi wa mbolea.”



Akizungumzia mafanikio kwa mwaka 2022/23, Dk Ngailo alisema TFRA  imefanikiwa kuimarisha  mifumo ya udhibiti wa mbolea na visaidizi vyake na kuwepo kwa ongezeko la wakaguzi wa mbolea kutoka wakaguzi 100 mwaka 2021 hadi 163 kufikia Juni 30 mwaka huu.



Alisema wamefanikiwa kuongeza usajili wa mbolea kutoka mbolea 240 mwaka 2018/19 hadi 507 mwaka 2022/23 wastani wa ongezeko la asilimia 22.3 kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano.



Aidha Dkt. Ngailo alisema pia kumekuwapo na ongezeko la idadi ya wafanyabiashara waliokaguliwa kutoka 1,000 mwaka 2020/21 hadi 3,081 hadi Juni 30 sawa na asilimia 84 ya lengo.



Pia kuimarika kwa mifumo ya upatikanaji na biashara ya mbolea nchini  kwa kuongeza wafanyabiashara kutoka 51 mwaka 2012/2013  na kufikia 4,562  Juni 30 mwaka huu.



Alisema Mamlaka imefanikia kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini kutoka tani 586,604 mwaka 2019/2020 hadi kufikia tani 1,115,841.

Kuimarika kwa mifumo ya upatikanaji na biashara ya mbolea nchini kutoka viwanda 4 mwaka 2016/2017 hadi kufikia viwanda 17 mwaka 2022/23 huku uzalishaji wa viwanda hivyo ukiongezeka kutoka tani 28,318 hadi tani 164,792 sawa na asilimia 25 ya mahitaji.

Dkt.Ngailo amesema Mamlaka   imeweza kujenga maabara ya kitaifa ya kudhibiti ubora wa mbolea na  ujenzi umekamilika na shughuli za uchambuzi wa mbolea zimeanza Julai 2023.

Kuhusu mbolea ya ruzuku, Dk Ngailo alisema  katika msimu wa 2022/2023 wakulima 3,369, 951 walisajiliwa  ambapo lengo la serokali ni kusajili wakulima milioni 7 ifikapo mwaka 2025.

Alisema kati ya wakulima hao waliosajiliwa, ni wakulima 949,643 ambao wamenunua tani 383,219.425.

 

No comments:

Post a Comment