AFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, amewataka watumishi wa BRELA kuutumia ushindi walioupata katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam kuwa ni chachu ya kufanya kazi kwa bidii na mshikamano.
Bw. Nyaisa ametoa wito huo mapema leo tarehe 17 Julai, 2023 katika Ofisi za BRELA Makao Makuu baada ya kukabidhiwa tuzo za ushindi na Mkurugenzi wa Leseni Bw. Andrew Mkapa ambaye alipokea tuzo hizo kwa niaba yake kutoka kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi wakati wa kufunga maonesho hayo Julai 13, 2023 katika uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere, wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
Bw. Nyaisa amesema kwa miaka mitatu mfululizo BRELA imekuwa ikipata ushindi katika kipengele cha Uwezeshaji na kukuza biashara na uwekezaji, kwani katika maonesho ya 45 ilipata ushindi wa tatu, ya 46 ushindi wa pili na sasa ya 47 ushindi wa kwanza, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuendelea kuwa wa washindi na hata kuwa washindi wa jumla wa maonesho yanayofuata.
“Nimefurahi BRELA kuwa washindi wa kwanza katika kipengele cha uwezeshaji na kukuza biashara na uwekezaji na ushindi huu umeleta changamoto kwa taasisi nyingine na kuhoji ni mkakati gani uliotumika na kutuwezesha kuwa washindi nina Imani kuwa ni team work ndiyo iliyotufikisha hapa”, amefafanua Bw. Nyaisa.
Amewataka watumishi kutobweteka na ushindi huo bali kujipanga zaidi ili kuhakikisha kuwa BRELA inabaki kufanya vizuri katika kipengele hicho , ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii, kutoa huduma bora na kuwajali wateja wakati wote.
Aidha, Bw. Nyaisa amesisitiza kuwa ili kuendelea kung’ara na kutunza taswira ya Taasisi watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na kila mmoja kuelewa kuwa asipofanya kazi vizuri ataathiri wengine. Hivyo ni lazima kila mmoja kujitambua na kufahamu kuwa kazi anayoifanya ina mchango mkubwa na asipoifanya vizuri ina athari kwa mwingine.
Vilevile amewaasa watumishi kuwa na nidhamu kwakuwa nidhamu ndio msingi mkuu katika utendaji kazi na kila mmoja aheshimu nafasi aliyopewa katika utumishi wake na kwamba njia bora kwa BRELA kuonekana inajali wateja na inahudumia wateja wake ni kuhakikisha inatoa suluhu ya maswali na mahitaji yao kwa wakati.
“Tunapaswa kuepuka urasimu usiokuwa wa lazima katika utendaji wa kazi na utoaji wa huduma zetu ili kukidhi matakwa ya wateja wakati wote ambao ni sekta binafsi na za umma”, amesisitiza Bw. Nyaisa.
Bw. Nyaisa amewapongeza watumishi wote pamoja na timu iliyoshiriki katika maonesho na kuwahakikishia kuwa ushindi huo ni wa watumishi wote kwani kila mmoja kwa nafasi yake amechangia na kuhakikisha kuwa ushindi umepatikana, hivyo watumishi waendelee kufanya kazi kwa bidii zaidi na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Mbali na ushindi wa kwanza BRELA pia imepokea cheti cha ushindi wa nne wa jumla katika mabanda bora pamoja na tuzo ya kutambuliwa kwa mchango wa waliodhamini Maonesho ya mwaka 2023.
ReplyForward |
No comments:
Post a Comment