Askari wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Songea akimvesha sare Diwani wa Kata ya LILAI, Simon Kapinga baada ya kuchagiliwa kwa kura 18 kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Simon Kapinga akitoa neno la shukrani kwa madiwani kwa kumuamini kushika nafasi hiyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Menas Komba, akitangaza matokeo ya Uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simon Kapinga.
NA STEPHANO MANGO, SONGEA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Songea limemchagua tena Diwani wa Kata ya Lilahi ML Simon Boniface Kapinga kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja wa fedha wa 2023/2024
Uchaguzi huo umefanyika kupitia Mkutano Mkuu wa mwaka wa Baraza la Madiwani 2022/2023 uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Lundusi ikiwa ni utaratibu wa kisheria wa kuchagua Makamu Mwenyekiti kila mwaka na uundaji wa Kamati mbalimbali za kudumu za Halmashauri.
Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Menas Komba amesema kuwa wajumbe waliopiga kura walikuwa 18 hivyo, Kapinga alishinda kwa kishindo kwa kupata kura zote 18 za ndio.
Komba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matimira, amesema kuwa Kamati zilizoundwa ni kamati ya Maadili, kamati ya kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango, Bodi ya Ajira pamoja na Kamati ya Ugawaji Ardhi.
Amesema kuwa madiwani wote wana haki sawa ndani ya Halmashauri hiyo, hivyo kila mmoja anawajibu wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya Mwaka 2015 na sio vinginevyo
Ameongeza kuwa ni lazima madiwani wakawa kiungo kizuri kati ya wananchi na Serikali yao kwani wao ndio wawakilishi ambao walipewa dhamana katika uchaguzi.
Pia ameeleza kuwa miradi ambayo inaibuliwa na wananchi kisha Serikali kuleta fedha, inapaswa isimamiwe kikamilifu ili matokeo yake yaweze kuonekana kwa ustawi wa wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Makamu Mwenyekiti na Wenyeviti wa Kamati zilizoundwa wameshukuru wajumbe wa kikao na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Songea inasonga mbele.
No comments:
Post a Comment