Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati wa Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere – Kibaha Mkoa wa Pwani tarehe 26 Agosti, 2023.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),
Dkt. Selemani Jafo, ametoa rai kwa wakuu wa mikoa kuifanya ajenda ya usafi
wa mazingira kuwa ya kudumu.
Ametoa wito huo Agosti 26, 2023 wakati akizungumza wakati wa
Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yanayofanyika
katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Dkt. Jafo amewataka wakuu hao wa mikoa kuzielekeza Mamlaka
za Serikali za Mitaa zilizo chini yao kusimamia vyema zoezi la usafi wa
mazingira katika maeneo yao ili kuifanya miji kuwa safi.
Alisisitiza kuwepo na utaratibu maalumu wa kujisaidia (kuchimba
dawa) kwa abiria wanaosafiri kwa mabasi badala ya porini kama unavyofanyika kwa
baadhi ya mabasi hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira.
Aidha, Waziri Jafo aliwataka wakuu wa mikoa hao kusimamia suala
la upangaji wa miji katika maeneo yao ili uwekezaji usikwame kutokana na
changamoto za kimazingira.
Alisema kuwa bila kupanga miji vizuri uwekezaji unakuwa ni
changamoto kubwa kwani itawalazima wawekezaji kusubiri kupata Cheti cha
Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kabla ya kuanza hatua ya ujenzi wa
miradi.
“Mtu atataka kujenga kiwanda katika makazi ya watu, mambo
yanakuwa yanaingiliana na mwisho wa siku wakati mwingine EIA zinachelewa
kwasababu tumeshindwa kufuata utaratibu wa mipango miji hivyo, tuwasisitize
watu wetu wa mipango miji kuhakikisha wanapanga vizuri miji yetu kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi,” alisisitiza.
Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Jafo
aliwahimiza viongozi hao kuendelea kusimamia zoezi la upandaji wa miti milioni
1.5 kwa mwaka katika kila halmashauri wanazozisimamia ili hifahi ya mazingira
iwe endelevu.
No comments:
Post a Comment