Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB – Filbert Mponzi (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom wakizindua ushirikiano kati ya benki ya NMB, Vodacom na Google wenye lengo la kutoa mikopo ya simu janja kwa Wateja wa Vodacom kupitia MPesa. Ushirikiano huo unaoitwa “Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo unaendana na maono ya serikali ya kuongeza matumizi ya digitali nchini.
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imeanzisha ushirikiano na kampuni za Vodacom Tanzania na Google unaotarajiwa kuimarisha mapinduzi ya kidijitali kwa kuwezesha upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu nchini.
Kwa kulipa kiasi cha kuanzia cha shilingi elfu 20, wateja wa Vodacom wenye vigezo watapata simu janja zinazoweza kutumia mtandao wa 4G na hivyo kuwawezesha kunufaika na fursa zinazopatikana mtandaoni.
Mpango huo mpya uitwao "Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo" kwa ushirikiano NMB na Android (mfumo wa uendeshaji wa Google kwa vifaa vya mkononi) unaenda sambamba na dira ya serikali ya ujumuishi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB Filbert Mponzi alisema sababu kubwa ya ushirikiano huo, ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufikia malengo ya kidijitali yanayojenga jamii jumuishi kwa ajili ya maendeleo endelevu.
“Tunaimani kuwa mpango huu utarahisisha upatikanaji na kuongeza umiliki wa simu janja ambazo zitawasogeza zaidi Wateja wa Vodacom katika ulimwengu wa kidigitali na kuanza kuchagiza uchumi wa nchi,” alisema Mponzi.
Mponzi alisema kulingana na matokeo ya utafiti wa Finscope Tanzania, takribani asilimia 75% ya Watanzania wanamiliki simu ila asilimia 19% tu ndio wanaomiliki simu janja yaani smart phone.
“Kama mnavyofahamu kuwa benki ya NMB tunayo kampeni yetu ya ‘Teleza Kidijitali’ ambayo inalenga kufikisha huduma rasmi za kibenki kwa watanzania wengi zaidi. Nina imani ushirikiano huu utaongeza kasi ya kurahisisha huduma za kifedha kiganjani na hivyo kuongeza idadi ya watanzania wanaopata huduma rasmi za kibenki,” aliongeza.
Naye Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni ya Vodacom Tanzania Hilda Bujiku wakati wa hafla hiyo alisema dhamira ya kampuni yake ni kuipeleka Tanzania kwenye ulimwengu wa kidijitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia.
“Ushirikiano huu unaenda sambamba na adhma yetu ya kuwafungulia wateja wetu fursa zinazobadilisha maisha. Tunaamini kwamba ushirikiano huu utaleta mageuzi katika upatikanaji wa simu janja kwa wale ambao bado hawajanufaika na zana hizi za kidijitali. Vodacom imeazimia kuwezesha wateja milioni moja kumiliki simu janja zenye uwezo wa 4G katika mwaka huu wa fedha pekee, na hivyo kuchangia kupunguza pengo kati ya wanaotumia na wasiotumia intaneti nchini" alisema Bujiku.
Bujiku alisema mikopo ya simu ni mbinu inayowezesha umiliki wa simu janja kirahisi na kwa gharama nafuu kupitia malipo ya siku au ya wiki kwa kima kidogo cha hadi shilingi mia tisa huku mtumiaji akifurahia manufaa yanayokuja na kuunganishwa kidijitali.
“Ushirikiano huu utatumia uwezo mpya wa kipengele cha kusimamia vifaa kwenye mfumo wa uendeshaji wa Android,” alisema.
Martin Njoroge Mkuu wa Android na Ushirikiano wa Kimajukwaa, Afrika Mashariki wakati wa hafla hiyo alisema lengo la Android daima nikuwawezesha watu kupitia huduma za kikompyuta.
“Ufikiaji wa fursa zilizo kwenye intaneti ni muhimu sana kwa ukuaji wa kiuchumi na ujumuishaji wa kijamii katika nchi yoyote ile. Tunaamini kwamba ushirikiano huu utawaleta Watanzania wengi mtandaoni na kuwasaidia kutumia fursa zinazopatikana mtandaoni,” alisema Njoroge.
Kwa maelezo zaidi kuhusu Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo, wateja wa Vodacom wanahimizwa kubonyeza *150*00# > 5 > 5 > 6 au kupiga namba ya huduma kwa wateja kupitia nambari 100 ili kupata maelezo zaidi.






No comments:
Post a Comment