NA JACOB KASIRI, IRINGA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
kupitia Idara ya Mahusiano kwa Jamii (Ujirani Mwema) katika Hifadhi ya Taifa
Ruaha imekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 31 kwa ajili
ya mradi wa maji safi na salama unaotarajia kuanza hivi karibuni ili kumtua
mama ndoo kichwani na kumpunguzia hadha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma
hiyo. Zoezi la kukabidhi vifaa hivyo limefanyika Agosti 31, 2023 katika kijiji
cha Tungamalenga kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Vifaa hivyo vilivyonunuliwa na TANAPA ni pamoja na
mipira ya kupitishia maji (GS Pipe medium na Polly pipe 63 mm) kwa ajili ya
kutandazia chini zaidi ya kilometa 2 na vifaa vingine vya mradi wote. Wanufaika
wa mradi huo wamechangia nguvu kazi kwa kuchimba mitaro na shilingi milioni
3.2. Shirika linaamini mradi huo utakapokamilika unapunguza changamoto ya
ukosefu wa maji katika kijiji hicho.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Kamishna Msaidizi wa
Uhifadhi Godwell Meng’ataki, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema "ninayo
furaha kubwa kutoa vifaa hivyo ikiwa ni faida inayotokana na utalii, hivyo
naahidi kushirikiana nanyi hadi mradi huu utakapokamilika."
"Kwa takribani miaka 12 TANAPA imetekeleza
miradi mingi sana. Kama shirika tumetekeleza miradi yenye thamani ya shilingi
bilioni 13 ikihusisha miradi zaidi ya 327 ya afya, elimu,maji na mpango wa
matumizi bora ya ardhi kijiji cha Tungamalenga kikiwa ni miongoni mwa vijiji
hivyo. Kwa mantiko hiyo tunawajibika kwa wananchi kutekeleza miradi ili
kuwapunguzia adha", alisema Kamishna Meing’ataki.
Hata hivyo, Kamishna huyo aliongeza
"tunapokabidhi vifaa hivi tujue msingi wake mkubwa ni uhifadhi.
Tunaposhirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi hawa katika uhifadhi na
kuibua miradi kama hii, tunapata faraja kama shirika kuona wananchi wanatambua
thamani ya Maliasili zao".
Aidha,Naibu Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Steria
Ndaga, Mkuu wa Kanda ya Kusini aliwaambia wananchi hao licha ya kukabidhiwa
vifaa kwa ajili ya mradi wa maji, kijiji cha Tungamalenga ni wanufaika zaidi wa
miradi mingine ya ujenzi wa madarasa na nyumba mbili za walimu walizojengewa
hivyo wailinde na kuitunza, pia aliwataka wawe mstari wa mbele kufichua vitendo
vya ujangili vinavyoendelea katika hifadhi hiyo.
Akikabidhi vifaa vya mradi wa maji safi na salama
kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Veronica Kessy, Katibu Tawala Bw.
Michael Semindu alisema, "kukamilika kwa mradi huu utaondoa changamoto ya
maji hapa. Najua tanki lililopo lina ujazo wa lita 60000 na lilijengwa
takribani miaka 20 iliyopita kipindi idadi ya watu ilikuwa ni chini ya 2500,
kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kijiji hiki kina zaidi ya wananchi
3600. Niwashukuru Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kutambua adha hii"
Kulingana na taarifa ya Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Afya,mtu mmoja anatakiwa atumie maji lita 50 kwa
mahitaji yake yote ya msingi kwa siku. Hivyo uwiano uliopo katika kijiji
chaTungamalenga hakikidhi matakwa ya umoja wa Mataifa, hivyo TANAPA imeona ni
vema kutekeleza mradi huo ili kutatua adha ya maji safi na salama.
Mmoja wa wanufaika Bi. Jennifer Joseph hakusita
kuonyesha furaha na hisia zake aliposema " shida ya maji kwetu ni tatizo
kubwa na la muda mrefu, unaenda kuteka maji umbali mrefu ukirudi nyumbani muda
wa wanafunzi kurudi kula unakuwa umetimia na hujaanda chakula na kusababisha
watoto kurudi shule bila mlo wa mchana. Tunawashukuru TANAPA kwa kutuondolea
kero hii".
"Kwa hiki tunachokishuhudia kukabidhiwa vifaa
hivi tunaahidi kuilinda Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa nguvu zetu zote, kwa wale waliokuwa
wanakula nyamapori na kuiita mchicha tutawasemea bila woga," aliongeza Bi.
Jennifer.
Kijiji cha Tungamalenga ambacho wananchi wake ndio
wanufaika wa mradi huo kiko takribani kilometa 20 kutoka Lango kuu la Hifadhi
ya Taifa Ruaha.
CR- MICHUZI
No comments:
Post a Comment