Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,
Alhaji Hasani Kabeke (kuhoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) leo kuhusiana na kupandishwa hadhi Msikiti wa Masjid Noor kuwa wa
Wilaya ya Nyamagana.
NA BALTAZAR MASHAKA,
MWANZA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, limesimika uongozi wa
Msikiti wa Masjid Noor na kukemea baadhi ya taasisi zilizo chini ya baraza hilo
zinazosababisha mgogoro na uvunjifu wa amani kwa kusajiliwa katika taasisi
mbili tofauti.
Limesema haliko tayari hata kwa dakika moja kupoteza dhiraa (kipimo cha mkono
kuanzia vidoleni hadi katika kiwiko)moja ya ardhi yake inayoisimamia na
kuwataka Waumini wa Dini ya Kiislamu wakiwemo wa Msikiti wa Noor,wasilishwe
matango pori na wasioitakiwa nchi amani na Uislamu.
Hayo yameelezwa leo na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, wakati
akitoa ufafanuzi kuhusu kusimikwa kwa uongozi wa Msikiti Masjid Noor uliopo
Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza, kupandishwa hadhi kuwa wa Wilaya ya Nyamagana.
Sheikhe Kabeke amesema msikiti huo umepewa hadhi kuwa wa
Wilaya na Baraza la Masheikhe la Wilaya Nyamagana na kumpendekeza Sheikhe Musa
Bin Rajab wa Msikiti wa Mabatini,kuwa Imamu wa msikiti huo kutokana na Sheikhe
wa Wilaya hiyo kutingwa na majukumu mengi.
Amesema BAKWATA ikishirikiana na vyombo vyake waliamua kwenda
kuswali Msikiti wa Masjid Noor kwa nia ya kuwafahamisha waumini kuwa msikiti
huo unaomilikiwa na BAKWATA kwa mujibu wa sheria,umepandishwa hadhi kuwa wa
Wilaya ya Nyamagana.
Sheikhe Kabeke amesema BAKWATA hawana tatizo isipokuwa jambo
lilipo wanatofautiana nani aongoze hapo na hawana sababu ya kutumia nguvu kubwa
na kuhoji kwa nini watumie nguvu na kwa jambo gani ilhali wao ni wamiliki?
Kwa masikitiko makubwa amesema vyombo vinavyosajili taasisi
za dini kuna hila na ujanja ujanja unafanyika na haelewi vinaitakia nini nchi
hii,kama vinaitakia mema huo mchezo unaoonekana si Mwanza tu ni Tanzania
kote,kelele zipo za dhuluma katika shule na msikiti,kinatokea kikundi
kinajisajili,usajili wao unafanyika taasisi nyingine nje ya BAKWATA.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza amesema taasisi inayoonewa
sana ni BAKWATA,hivyo wameamua uonevu huo uondoke na ukome,mtu kwenda katika
msikiti wa BAKWATA akajisajili kisha anakwenda kwenye vyombo vingine vya
usajili anakubaliwa,huo ni kuleta mgororo na kuvuruga amani.
“Baraza limeona msikiti huu ulivyo utabaki kuwa wa Wilaya ya
Nyamagana na tunachopigania ni maslahi mapana ya Uislamu na Taifa letu,sote ni
raia tuwe na busara na jicho la tatu, asije mtu akapitia katika hili kuzua
mgogoro ambao haupo,Mwanza imetulia na vitu vya documentation (nyaraka) ni
vizuri vikazingtiwa,”amesema.
“Mtatusaidia (wana habari) kuwaelimisha Watanzania na
waislamu hasa wa Mbugani na Wilaya ya Nyamagana,ifahamike msikiti huo una
historia ndefu tangu East African Muslimu Wallfare Society,ni mali ya BAKWATA
wala haijakurupuka.The Register of Trustee Masjid Noor iliposajiliwa mwaka 2010
iliuchukua kuuendesha,”amesema.
Sheikhe Kabeke amevitahadharisha vyombo vya usajili wa
taasisi za dini vichukue tahadhari vinginevyo vinaleta fujo na kusababisha
migogoro vinaposajili taasisi iliyokwisha kusajiliwa katika taasisi nyingine.
“Chonde chonde tunawatahadharisha wanaosajili,amani ya
Tanzania kwanza, pia kuna dalili za kuwahamasisha waumini na kuwalisha matango
pori,wasilishwe sumu kuwa BAKWATA imevamia msikiti hapana,ni msikiti wao tangu
1970,”amesema na kuongeza;
“Kwa maslahi mapana ya amani,hata jeuri hii ya kudai mali yetu tunaifanya
sababu nchi imetulia,nchi ina amani huwezi kusema tu nataka mali yangu damu
inamwagika maana yake nini,kwanza unataka kuwaswalisha akina nani wakati damu
imemwagika.
“Pia heshima ya dini yenyewe na kwa nafasi yangu Sheikhe wa Mkoa waislamu hawa
wote ni wangu natakiwa kuwakumbatia kwa huruma,maslahi ya heshima ya amani na
dini yetu, msikiti ni wetu wenzetu hao wataendelea kuutumia kwa ibada.”
Kiongozi huyo wa kiroho amesistiza kuwa hawako tayari kupoteza hata dhiraa moja
ya ardhi wanayoimiliki na kuisimamia na Watanzania wafahamu ukweli utabaki
hivyo kuwa, mali ikiwa BAKWATA ni ya waislamu wote,Bodi ya Wadhamini itawasemea
na kusimamia mali hizo kwa niaba yao.
“Baadhi ya bodi sisemi kwa ubaya zipo zinazofanya vizuri,shida iliyopo bodi
zilizosajiliwa kwa ujanja ujanja zingine utakuta za familia moja,mapato
hayasomwi,vikao hawafanyi bodi zipo tu,kibaya zimesajiliwa katika kiwanja cha
BAKWATA,wanapata wapi ridhaa ya kujisajili katika taasisi zingine? Amehoji.
Sheikhe Kabeke amesema wamefikia hatua hiyo si kwa ubabe kwani nchi mihimili
mitatu (Serikali,Bunge na Mahakama), inaendeshwa kwa utawala wa sheria ambapo
kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na kutoa haki. Pia viongozi waliopewa
dhamana na BAKWATA wanajitambua na hawawezi kukimbilia polisi iwasaidie kudai
haki yao,wanaoona wanaonewa ama wamedhulumiwa waende,kwa sababu hawana mgogoro
wa ardhi bali ulikuwepo mgogoro wa uongozi wa msikiti na tayari umepatikana.
No comments:
Post a Comment