TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE YAOKOA SH. MIL 500 - MAGENDELA BLOG

Breaking

Recent-Post

ads header

Friday, November 24, 2023

TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE YAOKOA SH. MIL 500

     Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, akizungumza.

NA MAGENDELA HAMISI

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeokoa zaidi ya Shilingi Milioni 500 baada ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa 16 wakati wa mafunzo ya wiki moja ya kuwaongezea ujuzi madaktari wa kitanzania ambayo yametolewa  na wataalamu kutoka nchini Australia.

 Hayo yamebainishwa, Novemba 23, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, wakati akifunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa wagonjwa hao ambao wamefanyiwa upasuaji huo wapo watoto waliokuwa na tatizo la matundu kwenye moyo.

Dkt Kisenge pia amesema kwamba matibabu hayo umefanyika kwa watu wazima baadhi yao wamefanyiwa upasuaji wa mshipa mkubwa ambapo awali ilikuwa haifanyiki Tanzania kutokana na kukosa wataalam na wagonjwa walikuwa wakipelekwa India na kila mmoja Serikali ilikuwa ikigharamia sh. mil 60.

“Wagonjwa waliokuwa na tatizo la kupasuka mshipa mkubwa unaosambaza damu maeneo mbalimbali ya mwili tulikuwa tunawapeleka India na baada ya mafunzo haya ambayo madaktari wetu wamepata tunaokoa sh. mil 40 kwa mgonjwa mmoja aliyetakiwa kwenda nje kwa matibabu.

“Tutoe shukrani kwa Rais wetu, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika vifaa tiba na rasilimali watu inayosababisha wataalamu wa mataifa mbalimbali kuvutika kuja nchini kutoa mafunzo kwa madktari wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa wataalamu wanaokuja nchini kutoa mafunzo wamekuwa na kasumba ya kutaka kuona matokeo mazuri ya wagonjwa baada ya matibabu ikiwemo ya upasuaji na hiyo inatokana na uwepo wa vifaa tiba vyenye ubora na madaktari wenye utaalamu wa kutosha.

 Dkt Kisenge ameongeza kuwa kutokana na taasisi hiyo kufanya vizuri katika utoaji wa huduma zake kwa kipindi cha robo mwaka wamepata wagonjwa wa nje ya nchi 60, wakitoka katika mataifa ya Zimbabwe, Comoro, Congo, Malawi, Msumbiji.

“Jambo kubwa ambalo limetushtua ni kupokea wagonjwa wa moyo raia wa Ufaransa na Ujerumani waliokuja nchini kwa shughuli za kiutalii na kupatwa na changamoto ya moyo, waliletea hapa ambapo awali walikuwa wakikimbilia Kenya au Afrika Kusini, hali hiyo inaonesha kuwa tuko vizuri katika kutoa,” amesema.

Amesema kutokana na wimbi kubwa la wagonjwa kufika hapo, imefanya kuwa na upungufu wa vitanda jambo lililosababisha Serikali kuamua kuipata taasisi hiyo, Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam ili kuongeza nguvu ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa wa ndani na watalii wanaokuja nchini.

Ameongeza kuwa kutokana na maradhi hayo kukua kwa kasi wiki ijayo watakuwa Kigamboni kwa ajili ya kupima wananchi bure na kuwaomba wakazi wa maeneo hayo na jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.

Naye Dkt. Darren Wolfers ambaye ni miongoni mwa madaktari 23 waliokuja nchini kutoa mafunzo, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa vifaa kulinganisha na mataifa mengine ambayo wamekwenda kutoa mafunzo.

 “Tumefarijika kukuta vifaa tiba venye ubora sawasawa na nchini kwetu, jambo hili limefanya utoaji wa mafunzo yetu kuwa rahisi, hivyo tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji huu na tutaendelea kushirikiana nayo katika kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kwa madakatari wetu,”amesema.

No comments:

Post a Comment